MKUU wa Wilaya Dodoma, Patrobas Katambi, amempa siku tatu muigizaji maarufu nchini, Emmanuel Mgaya maarufu kama Masanja Mkandamizaji kujisalimisha kituo cha polisi Dodoma baada ya kuwahoji wananchi mkoani humo kuhusu uelewa wa virusi vya Corona (Covid-19) kwa njia ya utani.
Katambi ametoa agizo hilo leo Ijumaa, Aprili 3, 2020, na kusema kuwa inaonekana Masanja anafanya utani kwenye vita dhidi ya janga la Corona ambalo linatishia dunia. Hii ni baada ya kipande cha video kinachomwonyesha msanii huyo kupitia Radio Dutch Welle (DW) akiwahoji wananchi kuhusu uelewa wao juu ya Covid-19.
“Viongozi wetu Mheshimiwa Rais, Waziri Mkuu na kamati ya kupambana na maambukizi ya virusi vya corona wametangaza very serious kwamba tusifanye mzaha kwenye gonjwa la corona.
“Lakini kwa masikitiko makubwa kumetokea mzaha kwenye vita hii ambao umefanywa na mmoja wa watangazaji wa vyombo vya habari vya Magharibi, anaitwa Masanja Mkandamizaji. Amefanya utani kuhusu ugonjwa huu kuonyesha kwamba wananchi wa Dodoma hawana uelewa kuhusu corona akitumia term ya Covid-19.
“Sasa kwa mzaha huo, tunataka kujua malengo ya mzaha huo ni nini hasa, na ni kwa nini amefanyia Dodoma. DW kutoka Ujerumani mnafahamu ugonjwa huu na hata Kansela Angela Markel aliugua corona. Kwa nini vyombo hiyo havijafanya huko kwao? Kwa nini wamefanyia Tanzania?
“Kwa hiyo ninamtaka Masanja kufikia Jumatatu ijayo awe ameshafika kwenye ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Dodoma ama kwa Mkuu wa Mkoa au kwenye kituo cha polisi ili atueleze nini malengo yake kufanya mzaha huo kwa sababu tupo very serious kupambana na corona wala hatuwezi kufanya mambo ya mzaha kama haya,” amesema Katambi.