The House of Favourite Newspapers

Kisa Vicoba, Mke adaiwa…

0

MAKUBWA! Mke aliyetajwa kwa jina la Hawa Mussa (20), mkazi wa Yombo – Buza, Dar amelalamikiwa na mumewe Abdul Aziz, kwamba amekimbia kwenye ndoa yao baada ya kumfokea kwa kosa la kuchelewa kurudi kutoka kwenye Vicoba.

Akizungumza na mwandishi wetu juzikati jijini Dar, mume huyo alisema mkewe aliondoka nyumbani baada ya kumuonya kutokana na mwenendo wake kubadilika sanjari na kuwa na makundi ya marafiki wasioeleweka.

“Siku hiyo aliniaga anapeleka pesa kwenye Vicoba. Bila yeye kujua, mimi nilimfuatilia kwa nyuma, nikashuhudia kweli anaingia Vicoba.

“Wakati anatoka, nikajua anarudi nyumbani, nikatangulia. Nilipofika nikashangaa yeye hafiki. Ilikuwa saa moja usiku. Nikampigia simu kumuuliza, akaniambia yuko jirani. Baadaye akafika. Nilipomuuliza alikuwa wapi, hakujibu. Nikaingia ndani yeye akiwa nje,” alisema Abdul.

Aliendelea kusema kuwa, mpaka saa tatu mkewe alikuwa hajaingia ndani, akatoka kumwangalia, hakumkuta! Akampigia simu, haikupokelewa. Alipopiga kwa ndugu zake kuuliza kama alikwenda huko, walisema hajafika.

“Tangu siku hiyo alikuja kunipigia simu baada ya wiki moja, akaniambia yuko Moshi (Kilimanjaro), nisimtafute tena kwani ameamua kuondoka kwa vile sababu nimekuwa nikimfokea sana anapochelewa kwenye Vicoba.

“Niliwajulisha ndugu zake, nao  wakashangaa amefuata nini Moshi wakati kwao ni Kilwa (Pwani).

“Nimeishi naye kwa miaka minne. Tumeshazunguka sana sehemu za starehe mpaka mwenyewe akaniambia inatosha, sasa tukae tutengeneze familia, akanishawishi nimfungulie biashara ya duka la nguo za kike, nikafanya hivyo, tukafunga ndoa,” alisema Abdul.

“Ndoa yetu haina muda mrefu, tumefunga Mei, mwaka huu hapa Dar. Sasa sijui imekuwaje! Kuna muda nikimpigia simu akipokea nasikia muziki kama yuko klabu.

“Kama haitoshi siku moja nilimpigia ikapokelewa na mwanaume, akanijia juu na kunitukana akidai kama namtaka mke wangu nimfuate Manzese (Dar), nikamueleza kila kitu, hakunielewa.”

Abdul alisema kufuatia hali hiyo, alikwenda Kituo cha Polisi Buza kutoa taarifa ya kutorokwa na mkewe, akapewa faili namba BUZ/RB/1607/2015 TAARIFA. Pia akamshtaki mwanaume huyo kwa kumtukana kwa faili la kumbukumbu BUZ/1680/2015 LUGHA YA MATUSI.

“Nimejifunza mengi kupitia huyu mwanamke kwani kwa hatua aliyofikia naamini basi tena. Kikubwa naomba nirudishiwe mahari yangu shilingi laki 5)  nikiachana na zile gharama nilizotumia wakati wa ndoa,” alisema Abdul huku akisikitika.

Leave A Reply