Kisa Wabotswana, Gomes Avunja Mapumziko Simba

BAADA ya mapumziko ya siku mbili, kikosi cha Simba juzi Jumatatu kilirejea mazoezini kujiandaa na mchezo wa hatua ya kwanza wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Jwaneng Galaxy ya Botswana.

 

Mchezo huo utapigwa kati ya Oktoba 17 nchini Botswana na utakuwa wa kwanza kwa Simba baada ya kupisha mechi za timu za taifa zinazowania kufuzu fainali za Kombe la Dunia zitakazofanyika mwakani nchini Qatar.

Wachezaji walioanza mazoezi juzi ni wale ambao hawajaitwa kwenye timu zao za taifa huku wale walioitwa wakiruhusiwa kwenda kujiunga na wenzao.

Akizungumza na Championi Jumatano, Meneja Mkuu wa timu hiyo, Patrick Rweyemamu, alisema kuwa kikosi chao kilirejea kambini juzi sambamba na kuanza mazoezi ya pamoja.

 

Rweyemamu alisema timu hiyo ilianza mazoezi asubuhi kwa kufanya programu moja pekee kwenye Uwanja wa Boko Beach Veteran jijini Dar es Salaam.

Aliongeza kuwa katika mazoezi hayo, Kocha Mkuu wa timu hiyo,Didier Gomes, anapata ugumu wa kufanya maandalizi mazuri kutokana na kukosekana nyota wao 16 muhimu waliokuwepo kwenye majukumu ya timu zao za taifa.

 

“Nyota 16 wameitwa kwenye timu zao za taifa ambapo tisa wamejumuishwa Stars wakati saba ni wale wa kimataifa ambao wameitwa na mataifa yao.

“Jana (juzi) timu iliingia kambini baada ya mapumziko ya siku mbili baada ya kocha Gomes kupendekeza kuendelea na mazoezi kwa ajili ya kutengeneza fitinesi kwa wachezaji 11 waliobakia katika timu.

 

“Lengo ni wachezaji waliobakia na timu kutengeneza fitinesi, hivyo tunaendelea na mazoezi hayo kwa ajili ya mchezo wetu wa Ligi ya Mabingwa Afrika tutakaocheza dhidi ya Jwaneng Galaxy ya Botswana.

“Hivi sasa tunafanya mazoezi kwenye Uwanja wa Boko Beach na tangu tumerejea, tumefanya programu moja ya mazoezi ambayo tunaifanya asubuhi pekee,” alisema Rweyemamu.

Wilbert Molandi, Dar es Salaam702
SWALI LA LEO

Kupanda Kwa Bei ya Mafuta Nchini, Nini Kifanyike Kupunguza Bei?
Toa comment