KISA WIVU WA KIMAPENZI… BABU ADAIWA KUMPA KICHAPO BIBI

ARUSHA: Inasikitisha! Bibi aliyejulikana kwa jina la Ester Taiko (64), mkazi wa Kata ya Ilkiurei wilayani Arumeru jijini hapa, anadaiwa kupewa kichapo na mumewe, Christopher Shanguro (74).  

 

Katika tukio hilo lililojiri hivi karibuni maeneo hayo, bibi huyo alidaiwa kunusurika kifo baada ya kumwagiwa oil chafu usoni na kutaka kukatwa panga na mumewe huyo ambaye ana wajukuu wanaomuita babu. Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo la kusikitisha lililojiri majira ya saa 1:00 asubuhi, wawili hao walidaiwa kuwa kwenye ugomvi wa kugombea mali na wivu wa kimapenzi.

 

Mashuhuda hao walidai kuwa baada ya bibi huyo kupewa kichapo ilibidi akimbizwe hospitalini akiwa haoni na hajitambui ili kuokoa maisha yake. Ilidaiwa kwamba, mbali na kumwagia oil chafu, mzee huyo alidaiwa kumtishia mkewe huyo kwa panga. Ilisemekana kwamba, siyo mara ya kwanza kwa wawili hao waliofunga ndoa miaka ya 1990 kutibuana kwani kuna kipindi ‘walilianzisha’ hadi wakasuluhishwa na kanisa.

 

Katika mahojiano na Gazeti la Risasi Mchanganyiko baada ya kupata nafuu, bibi huyo alisema kuwa alifungua jalada la kesi ya shambulio la kudhuru mwili kwenye Kituo Kikuu cha Polisi Mkoa wa Arusha ambapo mumewe huyo alitiwa mbaroni.

Bibi huyo alimtuhumu mumewe kushindwa kumjali kwa kutomwachia pesa ya matumizi ya kujikimu hivyo kusababisha familia kulala njaa. Alisema kuwa, yeye na mumewe huyo walifunga ndoa miaka ya 1990 na kujaliwa watoto nane. Alisema miongoni mwa mali walizochuma pamoja ni nyumba nyingi za kupangisha, mashine ya kusaga mahindi, mifugo na mashamba.

 

Alieleza kwamba, mumewe huyo alianza kumtuhumu kuwa na uhusiano wa kimapenzi na watu wengine, jambo ambalo si kweli na kuacha kumpatia pesa za matumizi sambamba na kumpa kipigo kisichokoma. Kwa upande wake mtoto mkubwa wa familia hiyo, Grace Christopher, mkazi wa Kata ya Kiranyi alisema kuwa wazazi wake hao wamekuwa kwenye ugomvi wa muda mrefu kiasi cha kuiathiri familia yao.

 

Alisema kuwa aiku ya tukio alipigiwa simu na kupewa taarifa kuwa mama yake alikuwa amekimbizwa katika Hospitali ya Mkoa wa Arusha ya Mount-Meru baada ya kupigwa na baba yake. “Nimekuwa nikimsihi baba yangu kuacha ukali ikiwemo kumfanyia maombi, lakini amekuwa akimtaka mama aondoke nyumbani, jambo ambalo sisi kama watoto tumekataa,” alisema Grace.

 

Alidai kuwa baba yake amekuwa akimtuhumu mama yake kuwa amejimilikisha watoto ambao wamekuwa upande wake na kumfanya yeye ajione mpweke. Kwa mujibu wa Jeshi la Polisi mkoani hapa, mtuhumiwa huyo anashikiliwa katika Kituo Kikuu cha Polisi na anatarajiwa kufikishwa mahakamani kujibu shitaka linalomkabili.

Toa comment