The House of Favourite Newspapers

Kisa Yanga, Majimaji Yaongeza Dozi

Kikosi cha timu ya Majimaji.

KUELEKEA mchezo wao wa Kombe la Shirikisho, kikosi cha Majimaji kimelazimika kufanya mazoezi yake mara mbili kwa siku ili kuweza kujiimarisha dhidi ya wapinzani wao katika mchezo huo, Yanga.

 

Majimaji inatarajiwa kuvaana na Yanga, keshokutwa Jumapili kwenye Uwanja wa Majimaji katika hatua ya 16 Bora ya michuano hiyo ikiwa ni mara yao ya tatu kwa timu hizo kukutana ndani ya msimu huu.

 

Ofisa Habari wa Majimaji, Onesmo Ndunguru, amesema kikosi hicho kimejipanga vyema na kipo hatua za mwisho za maandalizi ambayo wamekuwa wakifanya asubuhi na jioni.

 

Ofisa huyo amesisitiza kuwa wamejipanga kupambana na lengo ni kuingia kwenye hatua ya nane bora ya michuano hiyo ambayo bingwa mtetezi atawakilisha nchi kimataifa.

 

“Majimaji imejipanga na sasa hivi imekuwa ikifanya mazoezi mara mbili kwa siku asubuhi na jioni, tunapambana kutokana na uimara wa vijana wetu, hakuna majeruhi kwenye timu na wachezaji wanafahamu umuhimu wa mchezo ndiyo maana wanajituma kwa bidii kuweza kupata matokeo,” alisema Onesmo.

 

Timu hizo zimekutana mara mbili katika Ligi Kuu Bara msimu huu, mchezo wa kwanza Songea ulimalizika kwa sare ya bao 1-1, wa pili Yanga ilishinda mabao 4-1 kwenye Uwanja wa Taifa.

 

Upande wa Meneja wa Majimaji ambayo inadhaminiwa na Kampuni ya Sokabet, Gogfrey Mvula aliongezea kuwa nia yao ni kupata ushindi katika michezo yao yote ya nyumbani akidai wataanza na Yanga ambao wanawajua vizuri.

Comments are closed.