The House of Favourite Newspapers

Kisutu: Yaliyojiri Kesi ya Tido Mahakamani Leo

 

ALIYEKUWA Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Tido Mhando,  amesomewa maelezo ya awali ya kesi ya matumizi mabaya ya madaraka inayomkabili katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu leo Februari 28,2018 mbele ya Hakimu Mfawidhi, Victoria Nongwa.

 

Tido  anayetetewa na wakili Ramadhani Maleta amekubali maelezo binafsi kwamba alikuwa Mkurugenzi Mkuu wa TBC mwaka 2006 hadi 2010,  alikuwa msimamizi wa shughuli za TBC japo si zote, pia amekubali kutoa maelezo kwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) na kuwa alifikishwa mahakamani Januari 26, 2018.

 

Tido anakabiliwa na mashtaka manne ya kutumia madaraka vibaya,  moja la kuisababishia Serikali hasara ya Sh887.1 milioni. Anadaiwa pia  Juni 16, 2008 akiwa Dubai, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), akiwa Mkurugenzi Mkuu wa TBC kwa makusudi alitumia madaraka yake vibaya kwa kusaini mkataba wa kuendesha na kutangaza vipindi vya televisheni kati ya TBC na Channel 2 Group Corporation (BV1) bila kupitisha zabuni kinyume cha sheria ya ununuzi, hivyo kuinufaisha BVl.

 

Shtaka la pili anadaiwa kutumia vibaya madaraka yake ambapo Juni 20,2008 alisaini makubaliano ya utangazaji wa digitali duniani kati ya TBC na BVI. Shtaka la tatu anadaiwa Agosti 11, 2008 na Septemba 2008 akiwa Dubai alitumia vibaya madaraka yake kusaini mkataba wa makubaliano ya ununuzi, usambazaji, kufunga vifaa vya usambazaji na mnara wa utangazaji kati ya TBC na BVI na kuifaidisha BVI.

 

Shtaka la nne, anadaiwa Novemba 16,2008 akiwa Dubai alitumia vibaya madaraka yake kusaini mkataba wa makubaliano ya kuendesha miundombinu ya utangazaji kati ya TBC na BVI na kuinufaisha BVI,  na katika shtaka la tano anadaiwa kati ya Juni 16 na Novemba 16,2008 akiwa Dubai aliisababishia TBC hasara ya Sh887.1 milioni.

Tido amekana mashtaka yanayomkabili na upande wa mashtaka katika kesi hiyo utaanza kutoa ushahidi Machi 28, 2018.

SIKU 100! Mwananchi Wamlilia Azory, Mkewe Anateseka!

Comments are closed.