The House of Favourite Newspapers

Kitenge: Nimetua Rasmi Wasafi FM

Maulid Kitenge ‘chumvi’

 

MTANGAZAJI maarufu wa Habari za Michezo Tanzania, Maulid Kitenge ‘chumvi’ ameweka wazi kuwa ameachana na Kituo cha Redio cha EFM na kujiunga Wasafi  FM inayomilikiwa na mwanamuziki, Diamond Platinumz.

 

Maulid Kitenge alikuwa mtangazaji wa EFM tangu mwaka 2015 akiwa kama Mkuu wa Idara ya Vipindi vya Michezo, huku akitangaza vipindi vya michezo vya Sports Headquarters na E-Sport, pamoja na kusoma magazeti kwenye Kipindi cha Joto la Asubuhi ndani ya EFM iliyoko Kawe Beach Jijini Dar es Salaam. Katika kile kilichoelezwa kuwa ni sapraizi kwa mashabiki,jana EFM walimtambulisha msanii, Elizabeth Michael ‘Lulu’ asubuhi kama  mbadala wa Kitenge na kuibua gumzo.

Spoti Xtra lilikuwa la kwanza kufi chua ishu ya Diamond kumalizana na Kitenge wiki kadhaa zilizopita walipokutana nchini Marekani kwenye dili zao. Kitenge ameliambia Spoti Xtra jana kwamba ni kweli ameachana na EFM juzi Jumanne na amejiunga rasmi na Wasafi  FM ambapo atakuwa akikiongoza Kipindi cha Michezo cha Sports Arena.

Kitenge ambaye amewahi kung’ara na Radio One, aliongeza kuwa, kipindi hicho kitaanza Jumatatu ijayo na kitakuwa kikiruka hewani kuanzia saa mbili hadi saa tano asubuhi.

 

“Ni kweli nimeachana na EFM na nimehamia Wasafi  FM ambapo kuanzia Jumatatu ya wiki ijayo nitakuwa nafanya Kipindi cha Sports Arena ambacho kitakuwa hewani kuanzia saa mbili hadi saa tano asubuhi, lakini pia nitakuwa nasoma magazeti kwenye kipindi cha asubuhi saa moja na nusu.

 

“Katika kipindi hicho nitakuwa na Yusuph Mkule na Mwanaidi Suleiman ambao nilikuwa nikifanya nao kazi EFM, pia nitakuwa na watangazaji wengine kama Edo Kumwembe na Ahmed Abdallah.

 

“Baada ya wiki moja nitakuwa natangaza kipindi kingine cha michezo kitakachoanza saa moja usiku,” alisema Kitenge ambaye pia ni mchambuzi wa Gazeti la Championi Ijumaa.

Comments are closed.