The House of Favourite Newspapers

KIUNGO MCONGO ATUA SIMBA USIKU MNENE

SIMBA chini ya mwekezaji wake, Mohammed Dewji ‘Mo’, imedhamiria kuwakomesha wapinzani wake. Hii ni baada ya juzi usiku kushusha kiungo mwingine fundi ambaye alitua airport kama ninja akiwa amejificha sara yake.

 

Timu hiyo msimu uliopita ilitumia bilioni moja katika usajili wake ambapo kwa msimu huu hali inaweza kujirudia tena kutokana na aina ya usajili ambao inaendelea kuufanya.

Simba inayoongozwa na kocha Masoud Djuma, raia wa Burundi, hadi sasa imeshafanya vurugu na kuzipata saini za washambuliaji, Meddie Kagere, Adam Salamba, Mohamed Rashid, Marcel Kaheza, Abdul Suleiman na kipa Deogratius Munishi ‘Dida’ pamoja na beki Pascal Wawa ambaye hata hivyo anaweza kuachwa.

 

Licha ya nyota hao bado habari mpya ni kwamba viongozi wamemuongeza kiungo fundi kutoka Kiyovu Sport ya Rwanda, Kakule Mighuen Fabrice raia wa DR Congo huku usajili mzima wa mido huyo ukipendekezwa na kocha Masoud Djuma.

Awali, Championi Jumatatu ambalo lilikuwa linajua mchongo mzima wa safari ya Mcongo, lilikuwepo katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) na kumshuhudia akitolewa kwa usiri mkubwa majira ya saa nane usiku huku kiwa ameziba sura na kukimbizwa haraka kwenye gari iliyokuwa kimsubiri.

 

Kiungo huyo mwenye uwezo wa kupiga mashuti ya mbali, ratiba yake ya kutua ilikuwa ni saa 9 usiku lakini viongozi wa timu hiyo wakambadilishia ndege muda mchache kabla ya kutoka Kigali, Rwanda kwa ajili ya kukwepa kuonekana.

Lakini janja hiyo ilibainiwa na Championi ambalo lilikita kambi muda mrefu katika maeneo ya uwanja huo na kufanikiwa kumuona akiingizwa kwenye gari fasta.

 

Mighuen alipokewa na mratibu wa Simba, Abbas Ally ambaye ndiye aliyemtoa uwanjani hapo baada ya kutokea Rwanda na kupitia Kenya kuchukua ndege ya Kenya KQ ambayo iliingia saa nane na dakika 25 za usiku.

Championi linafahamu Mighuen amekuja kufanya mazungumzo na timu hiyo ambapo kuna asilimia kubwa ya kusajiliwa kutokana na kupendekezwa na Djuma pia kanuni za Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuruhusu namba ya wachezaji wa kigeni kuongezeka kutoka saba hadi kufikia kumi.

 

Championi Jumatatu lilifanya jitihada za kutaka kuzungumza na kiungo huyo Mcongo lakini zilikwama baada ya yeye kutokuwa tayari kuzungumza jambo lolote lile huku akiwa ameficha sura yake ndani ya koti kubwa akiwa kwenye gari ndogo.

Iwapo dili la mchezaji huyo likifanikiwa kutimia, Mkongo huyo ataungana na viungo wengine Haruna Niyonzima, Mzamiru Yassin, Said Ndemla na Jonas Mkude katika kuitumikia timu hiyo kwa msimu ujao.

 

Championi lilifanikiwa kumpata Mkurugenzi wa Ufundi wa Rayon Sport ambao ni watani wa jadi wa Kiyovu, Mbelgiji Ivan Minnaert ambaye alisema kuwa iwapo Simba itafanikiwa kumsajili kiungo huyo itakuwa imelamba bonge la mchezaji kutokana na kuwa na uwezo mkubwa uwanjani.

Ibrahim Mussa, Said Ally na Lunyamadzo Mlyuka

Waandishi Wetu, Dar es Salaam

Comments are closed.