The House of Favourite Newspapers

Kiungo Simba Atamani Kucheza Na Sure Boy, Fei Toto, Awakataa Aucho na Bangala

0

KIUNGO wa kimataifa wa zamani wa Simba raia wa Ghana, James Kotei, ameweka wazi kuwa kama ataambiwa achague viungo wa kucheza nao kutoka Yanga, basi atawataja Feisal Salum ‘Fei Toto’ na Salum Aboubakar ‘Sure Boy’ na sio pacha ya Khalid Aucho na Yannick Bangala.

 

Sure Boy aliyejiunga na Yanga kwenye dirisha dogo la usajili msimu huu akitokea Azam, amekuwa na kiwango bora mara baada ya kupata nafasi kutokana na majeraha ya Aucho ambapo awali alikumbana na changamoto ya namba kutoka pacha ya Aucho na Bangala.

 

Pacha ya Bangala na Aucho imekuwa katika ubora mkubwa ndani ya Yanga msimu huu ambapo wachezaji hao ni mara yao ya kucheza kikosini hapo wakitua mwanzoni mwa msimu, ndiyo chaguo la kwanza mbele ya Kocha Nasreddine Nabi pindi wanapokuwa fiti.

 

Akizungumza na Spoti Xtra, Kotei anayeichezea DTB FC inayoshiriki Championship, alisema: “Kama utaniambia nichague wachezaji wawili kutoka Yanga wa kucheza nao kwenye nafasi ya kiungo, basi nitawataja Fei Toto na Sure Boy, kwangu hawa ni wachezaji ninaowafahamu vizuri, naujua uwezo wao kwa kuwa nimewahi kucheza nao.

 

“Kuhusu Aucho na Bangala, hapana, kwa sababu sijawahi kupata nafasi ya kucheza nao na siwajui vizuri, hivyo kwangu uchaguzi ni kwa Fei Toto na Sure Boy.”

 

Wakati Kotei akicheza Ligi Kuu Bara akiwa na Simba kwa takribani misimu miwili na nusu, amewahi kukutana na wachezaji hao pindi Sure Boy yupo Azam na Fei Toto akiwa Yanga walipocheza dhidi ya Simba katika michuano mbalimbali ikiwemo Ligi Kuu Bara.

STORI; JOEL THOMAS

Leave A Reply