Kiza Kinene: Ujio Mpwa Wa Nandy Na Nyimbo Za Mapenzi

FEBRUARI 3,  2019, mwanamuziki Nandy alichia video ya Hazipo, wimbo ambao umeandikwa na Jay Melody na kutengenezwa na studio za Epic Record chini ya prodyuza Ringtone. Katika kipindi cha miezi saba iliyopita, Hazipo umekuwa ni  miongoni mwa nyimbo bora za Nandy kwa mujibu wa mashabiki wake.

Ndani ya miezi saba hiyo, Nandy amekuwa akipitia kipindi kigumu katika maisha yake kufuatia kifo cha Ruge Mutahaba ambaye alitajwa kuwa mchumba wake. Haikutosha kusema Ruge alikuwa mchumba bali alikuwa ni mwanaume aliyebadili maisha na historia ya muziki wa Nandy.

Kifo cha Ruge kilimpa majonzi makubwa Nandy, ni wakati huo ambapo wimbo ‘Nikumbushe‘ alioufanya ‘cover’ ya wimbo ‘Wema Wako‘ wa Angel Bernard,  ulianza kuvuma kwa kasi na kutumika kwenye misiba mingine mingi. Video ya Nikumbushe iliachiwa Machi 20, 2018,  na mpaka sasa imetazamwa zaidi ya mara milioni 3.7. Nikumbushe ilifuatiwa na ‘Ninogeshe‘ ya  mwaka huo 2018, hii inabaki kuwa video ya Nandy yenye mafanikio makubwa ikiwa na zaidi ya watazamaji milioni 10 katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita.


Kwa muda ambao Nandy amekuwa katika kipindi cha kumkumbuka mtu aliyempa ujasiri wa kufanya mambo makubwa, amekuwa maarufu kwa nyimbo zenye uhusiano na Mungu tofauti na nyimbo zake zilizopita. Nikumbushe si wimbo pekee ambao Nandy aliutumia kuzielekeza hisia zake kwa Mungu japo hii ilitoka kabla ya tukio la msiba huo ambao uliigusa jamii nzima ya Tanzania.

Wimbo mwingine wa kumsujudia Mungu ambao Nandy aliuachia ni ‘Mimi Ni Wa Juu‘ ambao pia ni ‘cover’ kutokea kwenye wimbo halisi wa muimbaji wa nyimbo za Injili Joel Lwaga.

 Muda mrefu umepita bila muziki mpya wa Nandy kwenye ladha ambayo mashabiki walimzoea. Mwezi Septemba 2019 umekuwa mwanzo mwingine wa muziki wake Nandy bila Ruge ambaye anatajwa kuunyanyua muziki wa msichana huyo kwa asilimia nyingi.

Nandy amerudi kwenye kiwanda cha Bongo Fleva kwa nyimbo mbili ukiwemo Bugana ambao ameshirikiana na Billnass uliyoachiwa Agosti 30. Ijumaa ya Septemba 6,  Nandy aliiachia kolabo yake nyingine kutokea Kenya ambapo wakati huu ameshirikiana na kundi la SautiSol kwenye wimbo ‘Kiza Kinene‘ .Kiza kinene uliotengenezwa na prodyuza Kimambo, unakuwa wimbo rasmi wa kwanza wa Nandy kuimba mapenzi baada ya kupita muda mrefu akisikilizwa kwa nyimbo mbili zenye uhusiano na Mungu ambazo zimechukua nafasi kubwa kwa miezi saba iliyopita.

\Video ya wimbo huu iliyoongozwa na Justin Campos ipo #6OnTrending YouTube Tanzania.


Loading...

Toa comment