The House of Favourite Newspapers

KMC Kuvaa Jezi Maalumu Dhidi ya Azam

UONGOZI wa timu ya Manispaa ya Kinondoni (KMC) umesema kuwa umeandaa jezi zenye ujumbe maalumu zitakazovaliwa na wachezaji wa timu hiyo leo Ijumaa.

 

Jezi hizo ni maalum kwa ajili ya kuhamasisha Watanzania umuhimu wa kulipa kodi kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) katika mchezo wa FA dhidi ya Azam FC ili kumuunga mkono Rais John Pombe Magufuli.

KMC itashuka dimbani leo kwenye Uwanja wa Chamazi nje kidogo ya Jiji la Dar, kucheza na Azam FC katika mchezo wa Kombe la FA Hatua ya Nusu Fainali.

 

Akizungumza na Championi Ijumaa, Meya wa Manispaa ya Kinondoni, Benjamin Sitta amesema kutokana na kuhitaji kuunga mkono juhudi za Rais Magufuli katika ulipaji kodi, wameona ni vyema kuandaa ujumbe katika jezi watakazovaa wachezaji katika mchezo huo ili kuhamasisha mashabiki.

 

“Ili kumuunga mkono rais wetu, tumesema tutaweka maneno kuhamasisha Watanzania umuhimu wa kulipa kodi, hivyo tukawashirikisha TRA ambao wamekubaliana na sisi bila ya malipo yoyote na wachezaji watavaa jezi zenye ujumbe huo ambazo ni maalumu kwa ajili ya michuano hii tu,” alisema Sitta.

 

Aidha, katika hatua nyingine mwenyekiti wa timu hiyo, Kheri Misinga ameeleza hofu yake juu ya kuhujumiwa katika mchezo huo kutokana na muda wa mchezo kubadilishwa ikiwa imebakia siku moja tofauti na taratibu zilivyo huku Azam FC ndiyo waliowapigia simu wakati waliotakiwa kutoa taarifa ni Shirikisho la Soka la Tanzania (TFF).

 

Awali, mechi hiyo ilipangwa kuchezwa saa 10:00 jioni lakini ghafl a jana Azam waliwapigia simu na kuwaambia mechi hiyo itachezwa saa 1:00 usiku.

 

Pia ameelezea mipango yao juu ya ukarabati wa uwanja wao uliopo Mwenge ambao unatarajiwa kuanza kutengenezwa Desemba, mwaka huu na kudai kuwa unaweza kugharimu Sh bilioni 1 bila hosteli na Sh bilioni 3 iwapo kutakuwa na hosteli, kwa sasa bado wapo katika upembuzi wakifi kia muafaka wataweka wazi.

Comments are closed.