The House of Favourite Newspapers

KOCHA BARCA AANZISHA KAMPENI YA KUIMALIZA UNITED

 

 

BARCELONA inaendelea kuwa na msimu mzuri wa 2018/19, hadi sasa bado inayo nafasi ya kufanya kweli kwa kutwa mataji matatu makubwa msimu huu.

 

Nafasi hiyo wanayo katika Kombe la Mfalme (Copa del Rey) ambapo wameshaingia fainali, katika Ligi Kuu ya Hispania (La Liga) wanaongoza kwenye msimamo kwa tofauti ya pointi 10.

 

Kutokana na kuwa na nafasi kubwa kwenye sehemu hizo mbili, sasa wanaongeza nguvu katika Ligi ya Mabingwa Ulaya ambapo wanatarajiwa kukutana na Manchester United katika robo fainali.

 

Kuwa mbele kwa pointi 10 kunawapa nafasi ya kubadilisha kikosi chao mara kadhaa bila kuwa na presha ya kukaribiwa na wapinzani lakini kuelekea katika Ligi ya Mabingwa wanajua huko kuna kazi nzito.

 

Licha ya kuwa wanapewa nafasi kubwa ya kuitoa Man United katika michezo miwili ya mwezi ujao, bado wanaamini ni vema wakaongeza nguvu kuhakikisha wanapata ushindi katika michezo yote miwili.

 

Washambuliaji wao, Luis Suarez na Ousmane Dembele wapo nje kutokana na kuwa majeruhi lakini wanapatiwa matibabu kwa kiwango cha juu ili kuwa tayari kabla ya michezo hiyo ya Ulaya.

 

Kocha Mkuu wa Barcelona, Ernesto Valverde, ameelezwa kuwa amekuwa akipambana kuhakikisha kikosi chake kinakuwa imara kuelekea katika mchezo huo na kuna mipango kadhaa inafanyika kuwapa mapumziko wachezaji wake mastaa katika mechi za La Liga ili wawe fiti kabla ya kuivaa United.

 

Staa wao, Lionel Messi yupo katika majukumu ya timu ya taifa ya Argentina lakini imeagizwa acheze chini ya dakika 90 ili kutomchosha.

 

Suarez na Dembele haijawekwa wazi wanaweza kurejea lini japokuwa awali ilielezwa ni ndani ya siku 25 lakini wanaweza kurejea mapema kabla ya hapo

Comments are closed.