Kocha Mrundi: Ntibazonkiza ataibeba Yanga

 

KOCHA wa Timu ya Taifa ya Burundi, Ndayizeye Jimmy, amesema Saidi Ntibazonkiza ataibeba Yanga kwenye michuano mbalimbali kutokana na uzoefu wake. Ntibazonkiza anayecheza nafasi ya kiungo mshambuliaji, ni mali ya Yanga baada ya hivi karibuni kupewa mkataba wa miaka miwili.

 

Nyota huyo anayeitumikia Timu ya Taifa ya Burundi, katika mechi tatu za hivi karibuni, amefunga mabao manne na kumfanya kuwa mchezaji hatari zaidi.

 

Akizungumza na Spoti Xtra, Ndayizeye amesema: “Saidi ni mchezaji mzuri, naona Yanga wamepata mchezaji wa kiwango cha juu kwani amecheza ligi kubwa ikiwemo Uholanzi, Uturuki, Ufaransa pamoja na ya hapa Burundi.

 

 

“Nafahamu kiwango chake, ataisaidia timu yake ya Yanga, ana uwezo wa kucheza nafasi zaidi ya moja. “Uwezo wa kufunga na spidi aliyonayo itakuwa ni faida kwa Yanga ambao wanapambana kutafuta mafanikio, ni wakati wake sasa kuonesha kile alichonacho ndani ya ligi ya Tanzania ambayo ina ushindani mkubwa.”

CAREEN OSCAR, Dar

Toa comment