KOCHA msaidizi na viungo wa Yanga raia wa Afrika Kusini, Riedoh Berdien, ndiye amekabidhiwa majukumu ya kukinoa kikosi hicho kilichoanza maandalizi ya msimu mpya wa 2020/2021.
Timu hiyo imeanza maandalizi yake juzi Jumatatu jioni kwenye Uwanja wa Chuo cha Sheria, Ubungo jijini Dar es Salaam kikiwa na wachezaji wake 11 pekee waliojitokeza katika mazoezi.
Wachezaji baadhi walioanza mazoezi ya timu hiyo wapya ni Yassin Mustapha na Waziri Junior huku wengine wawili wakiwa na udhuru ambao ni Bakari Mwamnyeto na Zawadi Mauya.
Akizungumza na Championi Jumatano, Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano wa Yanga, Hassani Bumbuli alisema kuwa timu hiyo itakuwa chini ya Bardien hadi itakapompata kocha mkuu.
Bumbuli alisema kuwa uongozi bado unaendelea na mchakato wake wa kumpata kocha mkuu kwa kupitia CV walizozituma kabla ya kufanya mchujo na kumpata mmoja bora atakayetangazwa hivi karibuni.
“Timu hivi sasa ipo chini ya kocha msaidizi na viungo Berdien aliyebakishwa kwenye benchi la ufundi baada ya kuwaondoa baadhi ya viongozi akiwemo aliyekuwa kocha wetu mkuu Eymael.
“Hivyo kocha huyo ataendelea na majukumu yake hadi pale mchakato wa kumpata kocha mkuu utakapokamilika hivi karibuni baada ya kufanyika mchujo wa makocha 64 walioleta maombi yao ya kufundisha Yanga.
“Upo uwezekano mkubwa mchakato huo kukamilika ndani ya wiki mara baada ya kukamilika kwa taratibu zote, kikubwa tunahitaji kocha atakayekuwa bora,” alisema Bumbuli.
Jana pia kocha huyo aliendelea na mazoezi kwenye uwanja huo huku akionekana kuwa mkali sana kwa wachezaji ambao walikuwa hawafuati maagizo yake.
Stori na Wilbert Molandi, Dar es Salaam