Kocha Simba Atamba Kuwapiga Red Arrows Mapema Leo
PABLO Franco, Kocha Mkuu wa Simba SC, amesema ana dakika 180 za ushindi mbele ya Red Arrows ya
Zambia ili kutinga hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Mhispania huyo, leo Jumapili ana dakika 90 za kuiongoza Simba kuibuka na ushindi dhidi ya Red Arrows kwenye
Uwanja wa Mkapa, Dar, kabla ya Jumapili ijayo kurudiana Zambia ambapo zitatimia dakika 180 za kuamua hatma ya kucheza makundi.
Pablo ameliambia Spoti Xtra kuwa, amewaambia wachezaji wake wanachohitaji ni ushindi kwa kuwa wataanzia nyumbani ili wakifika ugenini wakamalize kazi.
“Huu mchezo dhidi ya Red Arrows ni mgumu na siwezi kusema tuna dakika 90 pekee, hapana, bali ni
dakia 180 za kusaka ushindi na nimewaambia wachezaji kwamba tunapaswa kuanza kushinda hapa nyumbani ili tukamalize kazi ugenini.
“Ni mchezo wangu wa kwanza kuwa kwenye benchi la ufundi tena Uwanja wa Mkapa ambao una rekodi nzuri. Niliangalia mchezo uliopita ambapo Simba ilipoteza, kuna jambo nimejifunza.
“Mashabiki wamekuwa wakipenda kuona matokeo mazuri na hilo ndilo ambalo ninahitaji hasa baada ya kupata
ushindi mzuri kwenye mchezo wa kwanza wa ligi dhidi ya Ruvu Shooting.
“Haina maana kwamba mbinu itakuwa ni ileile, hapana, kutakuwa na mabadiliko makubwa kuanzia kwenye kikosi
na namna ambavyo tutacheza kwani haya ni mashindano mengine kabisa ambayo tunashiriki tofauti na mchezo wetu uliopita,” alisema Pablo.
AJIBU, SAKHO, KANOUTE NDANI
Kwenye mazoezi ya juzi Ijumaa ambayo yalifanyika Uwanja wa Mkapa, nyota wote wa Simba walifanya ikiwa ni pamoja na Sadio Kanoute, Ousmane Sakho na Ibrahim Ajibu.
Nahodha wa Simba SC, John Bocco alisema makosa ambayo waliyafanya kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Jwaneng Galaxy na kufungwa 3-1, yamewapa somo kubwa.
“Mchezo uliopita tulipoteza mbele ya Jwaneng Galaxy ambapo tulikuwa tunahitaji kushinda, makosa ambayo
tuliyafanya tumeyafanyia kazi na tunahitaji ushindi mbele ya Red Arrows.
“Wachezaji tupo tayari na tunahitaji kupata ushindi, hivyo mashabiki waendelee kuwa nasi, tunaamini kwamba
mchezo utakuwa mgumu na ushindani mkubwa kwa kuwa tunawaheshimu wapinzani, tutafanya vizuri,” alisema Bocco.
Kuelekea katika mchezo huo wa leo, Kocha Pablo huenda akaanza na kikosi hiki; Aishi Manula,
Shomari Kapombe, Mohamed Hussein, Pascal Wawa, Henock Baka, Jonas Mkude, Rally Bwalya, Bernard Morrison, Hassan Dilunga, Meddie Kagere na Kibu Denis.
WAANDISHI: Marco Mzumbe,Lunyamadizo Mlyuka na Hawa Aboubkhari.
MWANDISHI WETU, Dar