Kartra

Kocha Simba: Mechi Ya Merrikh Itakuwa Ngumu Zaidi

MARA baada ya kuondoka kwa Kocha Mbelgiji Sven Vandenbroeck ndani ya kikosi cha Simba mambo yalionekana kuwa yatakuwa magumu kwa ambaye atakuja kuchukua mikoba yake.

 

Hiyo ilikuja kutokana na Sven kuipeleka Simba hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kishindo baada ya kuwaondosha Wazimbabwe, FC Platinum kwa kipigo kizito cha mabao 4-0 kwenye Uwanja wa Mkapa jijini Dar.

 

Mara baada ya muda Januari 24, Simba wakamtambulisha Kocha Mfaransa, Didier Gomes kuwa kocha wao mpya akisaini mkataba wa miaka miaka miwili, mmoja kwa msimu huu na mwingine ataongezewa kutokana na mafanikio yake ndani ya kikosi hicho.

Kocha huyo ameanza kwa kasi kubwa hasa kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kushinda mechi zake mbili, moja ugenini dhidi ya AS Vita bao 1-0 na dhidi ya Al Ahly bao 1-0 kwenye Uwanja wa Mkapa.Simba wanaongoza kundi lao la A wakiwa na pointi sita.

 

Kocha huyo amesaliwa na mechi nne za ligi hiyo hatua ya makundi ambapo anafunguka juu ya hesabu zake sambamba na mchezo wake uliopita dhidi ya Al Ahly.

 

KIPI KILIWAPA MATOKEO KWENYE MECHI NA AHLY?

“Kwanza ijulikane Al Ahly ni timu kubwa kwa hapa Afrika lakini kitu kilichotubeba ni kuwaonyesha uwezo wetu katika kila sehemu ya uwanja.“Tulijitahidi kupambana kila nafasi japo tulikuwa na udhaifu kwenye sehemu chache tu lakini tunazichukua na kuzifanyia kazi mchezo unaokuja.

 

UNAJIVUNIA USHINDI HUU?“

Ndiyo najivunia ushindi huu, haukuwa rahisi hata kidogo kuupata, tumepambana vya kutosha kufanikisha hili. Acha tujivunie tu.

 

POINTI SITA SASA, INAAMINISHA KWAKO?

“Pointi sita ni kitu kizuri kwetu kwa ajili ya wakati ujao, hadi sasa pointi hizo zinatufanya tuwe kileleni mwa msimamo wa kundi letu.“Jambo hilo ni zuri na linatupa kujiamini katika mechi zetu zijazo kwa sababu tuna pointi hizo kwa sasa.

MCHEZO UJAO UNAUFIKIRIAJE?

“Kuhusu hilo tuna muda mwingi wa kufikiria juu ya mechi ijayo, itakuwa mechi ngumu kwa sababu naijua hiyo timu. Lakini kwa sasa nadhani tunatakiwa kutojipa mawazo sana kuhusiana na mechi hiyo inayokuja.”Ikumbukwe kuwa mechi ijayo ya Simba kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika watacheza Machi 5, mwaka huu nchini Sudan dhidi ya Al Merrikh SC ambayo Gomes aliifundisha kabla ya kutua Simba.

 

ULIONAJE MCHANGO WA LUIS MBELE YA AL AHLY?

“Siyo Luis (Miquissone) pekee, kila mchezaji alipambana sana katika mechi hiyo kwa ajili ya kufanikisha matokeo ambayo tuliyapata mwisho.“Kila mtu uliona alivyopambana mwanzo hadi mwisho wa mchezo wetu ule na kupata ushindi muhimu, wote walionyesha viwango vyao,” anasema.Miquissone ndiye ambaye alifunga bao.

Stori: SAID ALLY, Dar es Salaam


Toa comment