The House of Favourite Newspapers

Kocha wa Al Ahly Aingiwa na Hofu Leo, Bocco Atoa Mbinu

0

 SIMBA imetamba kuwa kikosi chao kipo fiti na tayari kwa ajili ya kupata pointi tatu katika mchezo wa leo Jumanne wa hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika watakapocheza dhidi ya Al Ahly ya Misri.

Mchezo huo wa Kundi A, unatarajiwa kupigwa kuanzia saa 10:00 jioni kwenye Uwanja wa Mkapa jijini Dar es Salaam.

 

Timu hizo zote katika michezo yao ya kwanza zilipata pointi tatu, Simba ikiwa ugenini, iliichapa AS Vita bao 1-0, huku Al Ahly wakiwafunga Al Merrikh mabao 3-0.

 

Akizungumzia mchezo huo, Kocha Msaidizi wa Simba, Selemani Matola,alisema kuwa ni mchezo mgumu kwao kutokana na ubora waliokuwa nao Ahly, lakini wamejipanga kupata matokeo mazuri kwenye uwanja wa nyumbani.

Matola alisema wachezaji wote waliowasajili kwa ajili ya michuano hiyo wapo fiti kuwavaa Al Ahly.“Ni mechi ngumu lakini tumejipanga kupata matokeo mazuri nyumbani, wachezaji wote tuliowasajili kwa ajili ya michuano hii wapo sawa kuelekea mchezo huo,” alisema Matola.

 

Naye nahodha wa timu hiyo, John Bocco, alisema kuwa: “Tunawaheshimu wapinzani wetu, ni timu kubwa Afrika, lakini kwa mbinu tutakazoingia nazo kesho (leo), naamini tutapata ushindi.“

 

Wachezaji wote wapo tayari kupambana na kufuata maelekezo ya mwalimu watakayopata kwenye mazoezi yetu ya mwisho tutakayofanya leo (jana) jioni, niwatake mashabiki kujitokeza kwa wingi na kuwaamini wachezaji katika mchezo wetu huu ambao ni muhimu kupata ushindi.

”Kwa upande wa Kocha Mkuu wa Al Ahly, Pitso Mosimane, alisema: “Tupo hapa tukiwa tunaiheshimu Simba, tunaiheshimu kama timu kubwa Afrika, hatupo hapa kuidharau, hawa wamecheza ugenini na kuifunga AS Vita.

 

“Kikubwa tulichopanga ni kukusanya pointi mapema kwa ajili ya kufuzu hatua inayofuata,” alisema Pitso na kuongeza.“Niliwahi kumfundisha Matola nikiwa Super Sports (Afrika Kusini) na kesho (leo) ninatarajia kukutana naye akiwa kocha msaidizi wa Simba na mimi kocha mkuu Al Ahly.

 

“Nafahamu anazijua mbinu zangu vizuri za ufundishaji, lakini hiyo hainifanyi nimuhofie sana, nilimfundisha zamani na mbinu za soka zimebadilika.”

Mara baada ya kuzungumza na Waandishi wa Habari, Pitso na Benchi la Ufundi la timu hiyo waliingia kwenye Uwanja wa Mkapa utakaotumika katika mchezo huo kwa ajili ya kuukagua wakitumia dakika tano na baadaye kuondoka.

 

Waarabu hao kutoka Misri, wanashuka dimbani hapo wakiwa na kumbukumbu ya kupoteza kwa bao 1-0 dhidi ya Simba msimu wa 2018/19 hatua kama hii ya makundi.

Leave A Reply