The House of Favourite Newspapers

Kocha wa Makombe Anakuja Simba

0

BAADA ya uongozi wa Simba kutangaza kuachana na aliyekuwa kocha mkuu wa timu hiyo Mbelgiji Sven Vandenbroeck, imebainika kuwa uongozi wa timu hiyo upo katika mchakato wa kumshusha na aliyewahi kuwa Kocha Mkuu wa Klabu Anderletch ya Ubelgiji na Al Ahly ya Misri, René Weiler ili kuja kuchukua mikoba iliyoachwa na Sven.

 

Rene Weiler mwenye uraia wa Uswisi kwa sasa ana umri wa miaka 47 ambapo alistaafu kucheza mpira mwaka 2001 na alikuwa anamudu kucheza nafasi ya beki wa kati.

 

Chanzo chetu cha kuaminika kutoka ndani ya Simba kililiambia Championi Jumamosi kuwa, uongozi wa Simba kwa sasa upo katika mchakato wa kutafuta kocha mpya ambapo kupitia CEO wa timu hiyo, Barbara Gonzalenz amependekeza jina la aliyewahi kuwa Kocha wa Al Ahly, Rene Wailer kuja kuifundisha klabu hiyo.

 

Inadaiwa Barbara anaamini kuwa anaweza kumshawishi kocha huyo kwa kuwa ana ukaribu na Weiler uliojengeka baada ya CEO huyo wa Simba kuitembelea timu ya Al Ahly wakati kocha huyo alipokuwa akiifundisha timu hiyo.

 

“Uongozi tayari umeanza mchakato wa kumpata kocha mpya kwa kuwa Sven kama unavyofahamu ameondoka ghafla na haikutegemewa kama lingetokea kwa sasa timu ikiwa katika hatua ya makundi Afrika, hivyo kutokana na hili la timu kuwa katika hatua nzuri viongozi wanahitaji kupata kocha haraka iwezekanavyo.“

 

Hivyo, Mtendaji Mkuu wa Simba, ‘CEO’ Barbara Gonzalez yeye alipendekeza jina la aliyewahi kuwa kocha mkuu wa Anderletch ya Ubelgiji na Al Ahly, Rene Wailer ili kuja kuziba pengo a kocha Sven aliyeondoka.

 

“Sababu za Barbara kulipendekeza jina la kocha huyo ni kutokana na uwezo wake mkubwa wa kutwaa makombe lakini kwa kuwa kocha huyo na CEO kuwa na ukaribu mkubwa kutokana na kiongozi huyo kuwahi kuitembelea timu hiyo wakati huo kocha Weiler alipokuwa akiifundisha Al Ahly.“

 

Hata hivyo kama uongozi ukikubaliana itabidi kuangalia dau lake kwani akiwa Al Ahly alikuwa analipwa mshahara mkubwa sana wa Sh milioni 50 kwa mwezi, tukiafikiana kwa maana ya kupunguza kidogo hiyo fedha basi anaweza kuja na ikiwa tofauti basi tutaangalia sehemu nyingine,”kilisema chanzo hicho.Championi Jumamosi lilipomtafuta Barbara Gonzalez juu ya taarifa hizo simu yake haikuwa hewani kwa muda mrefu.

 

HUYU HAPA RENE WAILER

Rene Wailer kwa sasa yupo huru akiwa hana timu baada ya kufukuzwa kazi Oktoba mwaka jana na Al Ahly ambayo alijiunga nayo Agosti 2019 akifanikiwa kuiongoza timu hiyo katika michezo 44 akishinda michezo 34 akitoa sare michezo 8 na kupoteza miwili.

 

Kocha huyo pia akiwa na Al Ahly alifanikiwa kutwaa makombe mawili, alitwaa la Ligi Kuu ya Misri katika msimu wa 2019/20 na pia akishinda Kombe la FA la Misri huku katika Ligi ya Mabingwa Afrika akiifikisha timu hiyo katika hatua ya nusu fainali.

RAGE ATOA NENO

Mara baada ya Klabu ya Simba kutangaza kuachana na kocha wake Sven, aliyewahi kuwa mwenyekiti wa klabu hiyo, , Ismail Aden Rage amesema kocha huyo ameondoka wakati ambao timu ilikuwa inafanya vizuri hivyo atakayekuja anatakiwa kuwafunika wote waliopita.“

Kiukweli siyo maamuzi mazuri kwa kipindi hiki, lakini wakati mwingine tunatakiwa kukubaliana na vitu visivyokubalika, lakini ukitazama wakati huu Simba ilikuwa inafanya vizuri, kwahiyo kuondoka kwake kuna ulakini kidogo.

“Hivyo, kocha ambaye atakuja anatakiwa kuifahamu vema Simba, wachezaji na mazingira yote ya nchi yetu, hiyo itasaidia kwa upande fulani timu kukaa muda mfupi kabla haijaingia kwenye mfumo wake. Kwa mashabiki wa Simba tujifunze kunyamaza na tuendelee kuisapoti timu kwa wakati huu,” alisema Rage.

Leave A Reply