The House of Favourite Newspapers

Kocha wa Oman atua Simba

0

Nicodemus Jonas,
Dar es Salaam
WAKATI ikiendeleza kutoa vipigo uwanjani, nje ya hapo uongozi wa juu nao umeamua kuboresha benchi lao la ufundi kwa kumshusha kocha wa makipa kutoka Uarabuni.

Tangu kuondoka kwa kocha wa makipa, Mkenya, Idd Salim, aliyefungashiwa virago wiki chache zilizopita, yeye pamoja na kocha mkuu, Dylan Kerr, raia wa Uingereza, timu hiyo imecheza mechi sita bila kocha maalum wa makipa.
Rais wa Simba, Evans Aveva, ameliambia Championi Jumatano kuwa, kocha huyo wanamtarajia siku chache zijazo ili ‘ku-boost’benchi lao la ufundi akisaidiana na kaimu kocha mkuu, Mganda, Jackson Mayanja ‘Mia Mia’.
Aidha, kuhusu mbadala halisi wa Kerr kama kocha mkuu, Aveva alisema bado mchakato unaendelea na kuna rundo la wasifu ‘CV’ za makocha kutoka mataifa mbalimbali duniani.
“Tuna rundo la CV, wapo wanaotokea Kenya, Serbia, Uingereza na sehemu nyingine nyingi lakini safari hii tumeamua kuwa makini sana, tena sana, hatutaki kurudia makosa ya mwanzo. Tunataka kumpata kocha sahihi haswa na ndiyo maana kamati ya ufundi haitakiwi kuwa na pupa.
“Kwa kocha wa makipa nadhani ndani ya siku chache sana zijazo atafika. Anatokea Oman ila sijajua jina lake lakini anakuja kama kocha wa muda,” alisema kigogo huyo kutoka Kundi la Friends of Simba (F.o.S).

Leave A Reply