The House of Favourite Newspapers

Kocha wa Yanga Aitaja Siri ya Kuwang’oa Waarabu Nchini Tunisia Kombe la Shirikisho

0

KOCHA Mkuu wa Yanga, Mtunisia Nasreddine Nabi ameshangaa kuwaona watu kama wamefungwa katika mchezo wa kwanza huku akiwaambia mashabiki wa timu hiyo, kuwa wasikate tamaa bado wana nafasi ya kupata matokeo mazuri ugenini.

 

Kauli hiyo ameitoa jana wakati timu hiyo, inajiandaa na safari ya kuelekea nchini Tunisia kujiandaa na mchezo wa marudiano wa Play-Off wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Club African ya Tunisia.

 

Yanga katika mchezo wa kwanza wa michuano hiyo ambao ulipigwa Jumatano iliyopita kwenye Uwanja wa Mkapa jijini Dar es Salaam timu hizo zilitoka suluhu.

Akizungumza na Championi Jumamosi, Nabi alisema kuwa, kwake bado hawajatolewa na ana matarajio makubwa ya timu yake kufuzu hatua ya makundi ya michuano hiyo.

 

Nabi alisema kuwa matumaini hayo ya kufuzu anayapata kutokana na kutopoteza mchezo wa nyumbani zaidi ya suluhu ambayo kwao ina faida kubwa kuliko wapinzani wao.

 

Aliongeza kuwa anaendelea na maandalizi ya kikosi chake kwa kuziboresha baadhi ya sehemu zenye upungufu ikiwemo ya kiungo na ushambuliaji ili kuhakikisha anapata mabao ya kuwapeleka makundi.

 

“Kwangu hii mechi haijaisha nimeshangaa kuwaona watu wanaona kama tumefungwa, nakubaliana na suala moja tu tumeshindwa kushinda nyumbani.

 

“Lakini kwangu sare hii inatupa faida zaidi Yanga kuliko wapinzani wetu ambao wenyewe watacheza kwa presha kubwa ya kutuzuia tusifunge bao ambalo litakuwa na faida kwetu kuliko wao.

 

“Wanayanga kikubwa wanatakiwa kutuombea na kuungana kwa pamoja katika kipindi hiki tukiendelea na maandalizi ya nguvu ili kufanikisha malengo yetu,” alisema Nabi ambaye muda mwingi wakati kikosi hicho kikiwa kinaondoka jana Ijumaa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere sura yake haikuwa na tabasamu nzuri, ambapo akizungumzia hilo alisema kwa kifupi.

 

“Asante sana mashabiki, asante sana mashabiki.” Kisha akapunga mkono wakati akiingia ndani ya Uwanja wa Julius Nyerere kuungana na msafara wa viongozi pamoja na wachezaji.

 

Miongoni mwa wachezaji waliokuwa kwenye msafara huo ni; Yannick Bangala, Bakari Mwamnyeto, Djigui Diarra, Fiston Mayele, Bernard Morrison, Dickson Job, Kibwana Shomary, Heritier Makambo, Farid Muss ana Aboutwalib Mshery.

Stori: Wilbert Molandi na Lunyamadzo Mlyuka

#BREAKING: NDEGE ya PRECISION YAANGUKA ZIWANI BUKOBA, UOKOAJI UNAENDELEA..

Leave A Reply