The House of Favourite Newspapers

Kocha wa Yanga Ategua Mitego Ya Waarabu Uwanja wa Mkapa, Dar

0

 

Kocha Mkuu wa Yanga, Mtunisia Nasreddine Nabi.

KOCHA Mkuu wa Yanga, Mtunisia Nasreddine Nabi amewataka mabeki wake kutofanya makosa yasiyokuwa na ulazima nje ya 18 yatakayosababisha mipira ya adhabu golini kwao watakaovaana dhidi ya USM Alger ya nchini Algeria.

Hiyo ni katika kuelekea mchezo wa kwanza wa fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika utakaopigwa kesho Jumapili saa 10 kamili kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar. Mchezo wa pili utakuwa Algeria Juni 3.

Safu ya ulinzi ya Yanga inaongozwa na nahodha Bakari Mwamnyeto, Ibrahim Bacca, Dickson Job, Djuma Shaban na Kibwana Shomari ambao wamekuwa wakianza mara kwa mara katika kikosi cha kwanza.

 

Akizungumza na Championi Jumamosi, Nabi alisema anakwenda kucheza dhidi ya USM Alger akiwa anaifahamu vizuri kimbinu, wakitumia mipira ya kutenga kupata mabao faulo na kona.

Nabi alisema kuwa tayari amewaandaa mabeki hao ili kuhakikisha wapinzani wao hawapati faulo za nje ya 18 huku wakipunguza mipira ya kona ambayo ni hatari kwa USM Alger kuicheza kwa vichwa.

Mtunisia huyo alisema kuwa kingine amewataka mabeki wa pembeni kutoruhusu mipira ya krosi kupigwa golini kwao, kwa lengo la kutowapa nafasi ya kucheza mipira ya juu huku akiamini mbinu alizowapa kwa siku hizi tatu kambini Avic Town, Kigamboni kuwaandaa.

Aliongeza kuwa pia amewataka viungo wake wakabaji Mudathir Yahya na Yannick Bangala kutowapa nafasi ya kumiliki mpira viungo wa USM Alger ambao wameonekana wenye kasi na uharaka wa kupiga pasi zenye madhara golini kwao.

“USM Alger ni wazuri katika mipira ya ya kutenga, kwa maana ya faulo na kona hilo nimeshawaambia wachezaji wangu na kuwapa mbinu za uchezaji zitakazozuia mipango yao ya ushindi kwa kuanzia hapa nyumbani kabla ya kwenda kurudiana kwao.

“Maandalizi hayo niliyoyafanya yanatosha kabisa kwetu kupata ushindi, mabeki wangu nimewaambia wawakabe kwa makini na tahadhari ya hali ya juu wapinzani wetu ambao ninaamini watatumia muda mwingi kupoteza dakika, kwani ndio mbinu zao wanazozitumia wakiwa ugenini.

“Pia nimewataka viungo wangu kutowapa nafasi viungo wa wapinzani kumiliki mpira kwa muda mrefu, kwani watataka wapoteza muda kwa kukaa mpira, hapa nyumbani tunahitaji ushindi wa mabao mengi ili yawe faida tutakaporudiana.

“Katika mchezo huu tutamkosa Khalid Aucho, ni pengo lakini sio kubwa ninao wachezaji wengine uwezo wa kucheza na pengo lake kutoonekana akiwemo Bangala, Mudathiri na Mauya (Zawadi),” alisema Nabi.

SHIGONGO: ATOBOA SIRI ya MAFANIKIO YAKE USIKU wa YOUNG CEO “VIJANA MTAFUTE MAARIFA”

Leave A Reply