The House of Favourite Newspapers

Kocha wa Yanga Awabebesha Zigo Zito Lomalisa, Moloko

0

KOCHA Mkuu wa Yanga, Mtunisia Nasreddine Nabi anataka kuona timu yake ikitengeneza mabao kupitia pembeni ikiwatumia mabeki na viungo wa pembeni katika kupeleka mashambulizi golini kwa wapinzani wao.

Hiyo ni katika kuelekea mchezo wa marudiano wa hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika ambao Yanga watavaana dhidi ya US Monastir ya nchini Tunisia kwenye Uwanja wa Mkapa jijini Dar.

Mabeki wa pembeni wa Yanga ambao wanaanza katika kikosi cha kwanza hivi sasa ni Joyce Lomalisa, Djuma Shaban huku viungo ni Jesus Moloko na Kennedy Musonda ambaye ni mshambuliaji wa kati lakini kocha huyo anamtumia pembeni katika michuano ya kimataifa.

Mmoja wa mabosi wa Yanga kutoka katika benchi la ufundi la timu hiyo, ameliambia Championi Ijumaa kuwa, katika program ya jana Alhamisi asubuhi kocha huyo aliwapa mazoezi maalum ya kiufundi na kimbinu mabeki wa pembeni, viungo wa pembeni na washambuliaji pekee.

Bosi huyo alisema kuwa, kocha huyo aliwataka mabeki hao pembeni kuanzisha mashambulizi kutokea nyuma kwa kupiga krosi na kona safi za juu na chini zitakazowafikia washambuliaji wake Fiston Mayele na Musonda kabla ya kufunga.

Aliongeza kuwa pia aliwapa program za kimbinu viungo wa pembeni jinsi ya kupiga krosi, kona na faulo watakazozipata katika mchezo huo ili wazitumie vizuri kwa kufunga mabao.

“Jana (juzi) kocha aliwaingiza gym wachezaji kwa lengo la kuwaongezea fitinesi ni baada ya kuona kuna tatizo fiziki, na leo (jana Alhamisi) katika program ya asubuhi aliwapa mazoezi ya kimbinu mabeki na viungo wa pembeni.

“Kocha anataka kuona mabeki na viungo hao wakipiga krosi na kona nzuri katika goli la wapinzani zitakazowafikia washambuliaji wake Mayele na Musonda.

“Mara kadhaa kocha ameonekana akisimamisha mazoezi na kutoa maelekezo kwa wachezaji wake pale wanapokosea na kucheza bila ya kufuata maelekezo yake, kuelekea mchezo huo ametaka kila kona, faulo na krosi itakayopigwa liwe bao,” alisema bosi huyo.

Akizungumzia hilo, Nabi alisema kuwa: “Tulichocheza ugenini dhidi ya US Monastir ni tofauti tutakapokwenda kukutana tena kwa mara ya pili sasa hivi tutakuwa nyumbani kwetu.

“Hivyo tutaingia kwa tahadhari kubwa ya kushambulia sana na kujilinda kidogo huku tukitumia mbinu mpya za ushindi wa nyumbani, nisingependa kuweka wazi mbinu tutakazozitumia hivi sasa,” alisema Nabi.

STORI NA WILBERT MOLANDI

UGONJWA ULIOUA WATANO KAGERA ni EBOLA? RC CHALAMILA AFUNGUKA – ”HAKUNA MGONJWA wa EBOLA”…

Leave A Reply