Kartra

Kocha Yanga SC: Simba Hii ni Hatari

ALIYEKUWA kocha wa magolikipa wa kikosi cha Yanga msimu uliopita ambaye kwa sasa anahudumu katika kikosi cha Kagera Sugar, Manyika Peter, amesema ni jambo lililo wazi kuwa Simba ya sasa iko kwenye kiwango cha juu sana.

 

Manyika juzi Jumamosi alikuwa sehemu ya benchi la ufundi la Klabu ya Kagera Sugar katika mchezo wa hatua ya 16 bora ya Kombe la Shirikisho dhidi ya Simba, ambapo Kagera Sugar walikubali kipigo cha mabao 2-1.

 

Kutokana na kipigo hicho Kagera Sugar sasa imeondolewa rasmi katika michuano hiyo na kuiacha Simba ikikata tiketi ya kutinga hatua ya robo fainali.

 

Akizungumza na Championi Jumatatu, Manyika alisema: “Kwa ufupi mchezo wetu wa Jumamosi dhidi ya Simba ulikuwa mzuri, tulicheza kwa nidhamu kubwa ya ulinzi katika kipindi cha kwanza, na kufanikiwa kupata bao la kuongoza huku tukiwa tumewazuia kabisa Simba wasipate bao.

 

“Lakini kipindi cha pili walifanya mabadiliko ya kuingiza wachezaji walio na mikimbio ya hatari wanapokuwa hawana mpira kama ilivyo kwa Bernard Morrison, ambao walizidisha presha kwetu na kufanikiwa kupata mabao mawili kuto¬kana na makosa tuliyofanya, lakini nikiri wazi kuwa Simba kwa sasa wako katika kiwango bora sana.”


Toa comment