The House of Favourite Newspapers

Koffi Olomide ahukumiwa Kwenda Jela Miaka 2

 

Koffi Olomidé, mmojawapo kati ya nyota wa muziki Afrika , amepatikana na hatia ya kumbaka mmoja ya wanengeuaji wake alipokuwa na umri wa miaka 15.

 

Amehukumiwa miaka miwili gerezani na mahakama ya Ufaransa akiwa hayupo, baada ya kukosa kufika mahakamani.

 

Uamuzi huo una maana kwamba nyota huyo wa Congo atakamatwa iwapo atafanya uhalifu mwingine, amesema mwandishi wa shirika la habari la Uingereza (BBC) Nadir Djennad.

 

Olomidé, mwenye umri wa miaka 62, aliagizwa alipe Euro 5,000 kwa madhara aliyomsababishia mnenguaji wake huyo wa zamani.

 

Mahakama ya Nanterre, nje ya mji mkuu Paris, pia ilimuagiza alipe faini ya kiwango sawa na hicho kwa kuwasaidia wanawake watatu wengine kuingia nchini Ufaransa kwa njia haramu.

 

Wakili wa Olomidé amepongeza uamuzi huo na kuutaja kuwa ushindi, akiwataarifu waandishi wa habari kwamba uamuzi huo utachangia kuondolewa hati ya kimataifa ya kumkamata popote alipo.

 

Koffi Olomidé ni nyota wa muziki wa mtindo wa rumba na soukous ambao ni maarufu sana barani Afrika. Olomidé alishtakiwa mara ya kwanza mnamo 2012 kwa ubakaji lakini mashtaka yakapunguzwa.

 

Wanenguaji wanne waliokuwa wakimfanyia kazi wameiambia mahakama kwamba aliwanyanyasa kingono mara kadhaa kati ya mwaka 2002 na mwaka 2006. Wameeleza kuwa unyanyasaji huo ulifanyika katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo na Ufaransa.

 

Wanawake hao pia walieleza kwamba walizuiwa kwa lazima katika nyumba moja nje ya mji wa Paris na walifanikiwa kutoroka usiku wa Juni 2006, lakini hawakurudi DR Congo kutokana na kuogopa kutafutwa na kulipizwa kisasi.

 

Waendesha mashtaka walikuwa wakishinikiza ahukumiwe miaka saba gerezani lakini mahakama imetupilia mbali mashtaka ya unyanyasaji na madai ya utekaji nyara.

 

Olomidé alikimbilia Congo mnamo 2009 akiahidi kujitetea lakini alikosa kufika mahakamani Ufaransa katika kesi hiyo ambayo kutokana na ombi la walalamishi ilifanyika faraghani.

 

Mwimbaji huyo ambaye jina lake halisi ni Antoine Agbepa Mumba, amekuwa akiingia matatani mara kwa mara kwa uvunjaji wa sheria.

Comments are closed.