Kolabo za Diamond kimataifa nani anafuata ?
Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’
ANDREW CARLOS
Haina ubishi kuwa staa wa Muziki wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ anazidi kukwea levo za kimataifa. Ameweza vema kuipeperusha bendera ya Taifa na sasa ukiongelea miongoni mwa wasanii wenye ushawishi ndani na nje ya Afrika Mashariki ni wazi utamjumlisha.
Hadi sasa ameshafanya kolabo nyingi za kimataifa na zote zimefanya vizuri kiasi cha kumpatia tuzo kibao kama vile Afrimma, Afrima, Kora, MTV Music (MAMA), MTV EMA huku jina lake likisoma kwenye tuzo kubwa duniani za BET.
Katika makala haya, yanaweka wazi kolabo zake za kimataifa;
DAVIDO (NUMBER ONE REMIX)
Kwa mara ya kwanza Januari 2014, Diamond alianza kujulikana nchini Nigeria na baadhi ya nchi za Afrika baada ya kuibuka na Ngoma ya Number One Remix akiwa amemshirikisha staa kutoka Nigeria, David Adeleke ‘Davido’ ambapo ngoma hiyo ilibamba vilivyo Afrika.
Iyanya (Bum Bum)
Kolabo na Davido ikiwa bado ipo hot, Julai, 2014 Diamond alidumbukia tena na ngoma mbili, Mdogo Mdogo pamoja na Bum Bum aliokuwa amemshirikisha staa wa muziki kutoka Nigeria, Iyanya.
BRACKET & TIWA SAVAGE
Desemba 2014, Diamond aliendelea kutengeneza vichwa vya habari Bongo, Nigeria na baadhi ya nchi jirani baada ya kuibuka katika kolabo ya Kundi la Bracket wakiwa pamoja na mwanadada Tiwa Savage.
Katika wimbo huo uliojulikana kama Alive ulikuwa maalum kumshukuru memba wa Kundi la Bracket, Vast ambaye alipona baada ya kuugua kansa kwa muda mrefu.
FLAVOUR (NANA)
Kuonesha kuwa bado wa kimataifa na kolabo nyingi zikiendelea kuvuka boda ya Afrika, Mei 2015, Diamond aliibuka tena na kolabo ya Ngoma ya Nana aliyoifanya na staa wa muziki kutoka Nigeria, Mr. Flavour.
Kcee na Diamond platnumz
KCEE ( LOVE BOAT)
Kolabo yake na Mr Flavour ikiwa bado hot, Juni 2015, Diamond alishirikishwa tena katika Ngoma ya Love Boat na staa mwenye mbwembe kibao kutoka Nigeria ambapo ngoma hiyo iliyojaa warembo kibao ilizidi kumpandisha chati.
AKA (MAKE ME SING)
Baada ya kufanya kolabo za kutosha hususan na wakali wa muziki wa Nigeria, Diamond alifanya ngoma za peke yake ambazo zilifanya vema na Februari, mwaka huu aliibuka kwa mara nyingine akiwa na staa wa muziki kutoka Sauz na Ngoma ya Make Me Sing ambapo video yake iligeuka kuwa gumzo kutokana na kuvaa uhusika wa kijambazi.
MAFIKIZOLO
Ni kama upepo wa kolabo upo Sauz, baada ya kufanya poa na Aka, hivi karibuni Diamond ameibuka tena na kuteka vichwa mbalimbali vya habari za burudani Sauz na Bongo baada ya kuibuka na kolabo ya Ngoma ya Colors of Africa aliyoshirikishwa na kundi linalobamba nchini humo la Mafikizolo.
P-SQUARE (?)
Kwa sasa pacha wanaounda Kundi la P-Square wapo Sauz wakitengeneza video ya wimbo wao mpya. Ikumbukwe kuwa Diamond alishawahi kukaririwa akisema kolabo yake na P-Square inakuja.
Bado haijaweka wazi ni ngoma gani lakini mmoja wa pacha hao, Peter hivi karibuni kwenye mitandao ya kijamii alionekana akiposti picha akiwa na kofia ya nembo ya Diamond huku akionesha dalili kuna kitu wanafanya pamoja huko Sauz.
NE-YO (?)
Hadi sasa kolabo aliyofanya na staa wa R&B kutoka Marekani Ne-Yo imeshakamilika ambapo audio aliitengenezea nchini Kenya,
Katika kolabo hiyo ambapo Machi, mwaka huu Diamond ilikuwa atengeneze video yake na staa huyo Marekani, bado haijajulikana lini itatoka japo ipo kwenye foleni.
KANYE WEST (?)
Akiwa katika moja ya safari zake za nje kufanya shoo, Diamond alikutana na Kanye West kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Los Angeles wa LAX nchini Marekani wakati akisubiri ndege kuelekea Las Vegas.
Na baada ya kukutana huko mbali na kupiga picha, inadaiwa kuna mipango ya kufanya naye kolabo siku za mbeleni.
Ikiwezekana hili atakuwa levo nyingine yaani kutoka Nigeria, Sauz hadi Marekani.