Na Elvan Stambuli
Leo tutatupia jicho baadhi ya tafiti zinazohusu ugonjwa wa saratani ya matiti. Uchunguzi mpya umeonyesha kwamba, katika tunda la komamanga kuna kemikali zinazozuia kansa ya matiti kusambaa mwilini.
Uchunguzi huo uliochapishwa katika Jarada la Utafiti la Kuzuia Kansa la China umeonyesha kwamba, kemikali ziitwazo ellegitannins zinazopatikana kwa wingi kwenye komamanga, zinaweza kuzuia kimeng’enyo (enzyme) aina ya aromatase, suala ambalo huzuia kukua kwa homoni ya estrogen inayopatikana katika kansa ya matiti.
Dk. Shiuan Chen aliyeongoza uchunguzi huo amesema kwamba, kemikali hizo hupunguza uzalishwaji wa estrogen, na kusaidia kuzuia seli za kansa ya matiti kuzaliana mwilini pamoja na tezi la ugonjwa huo kukua.
Aromatase ni kimeng’enyo ambacho hugeuza homoni ya androgen kuwa estrogen, na kushambuliwa kimeng’enyo hicho ndio lengo kuu la dawa za kupambana na kansa za matiti zinazosababishwa na homoni ya etrogen.
Huko nyuma pia uchunguzi ulionyesha kwamba tunda la komamanga lina faida kubwa kiafya hasa kwa kuwa na antioxidant nyingi na vitamini mbalimbali, ambazo hulifanya tunda hilo liweze kusaidia katika mapambano dhidi ya magonjwa ya saratani, matatizo ya moyo na hata ugonjwa wa kusahau uzeeni au Alzheimer.
Antioxidant huzuia radikali huru ambazo ni hatari sana kwa miili yetu. Uwezo huo huufanya mwili uweze kukabiliana na magonjwa mbalimbali hata ugonjwa wa homa ya mafua ya nguruwe.
Kutokana na faida nyingi za tunda hili, kama huwezi kulipata sokoni, basi unaweza kutumia juisi yake na daima kuitunza afya yako. Faida nyinginezo za juisi ya komamanga ni kwamba huzuia maendeleo ya saratani ya mapafu, hupambana na saratani ya matiti, hupunguza ukuaji wa saratani ya kibofu, inaweza kuzuia na kupunguza kasi ya ugonjwa wa Alzheimer na inapunguza mafuta mwilini pia hushusha shinikizo la damu na hulinda meno.
Ukinywa juisi ya komamanga (pomegranate) nusu lita kila siku kwa muda wa mwezi mmoja, inasaidia kupunguza mafuta tumboni kwa wale wenye vitambi.
Dk. Baroness Delyth Morgan, Mkurugenzi Mkuu wa Kampeni ya Kupambana na Saratani ya Matiti nchini Marekani amesema kuwa, kwa mara nyingine utafiti huo umesisitiza jinsi mfumo wa maisha ya mtu unavyoweza kuathiri hatari ya kupata ugonjwa wa kansa ya matiti.
Wataalamu wamegundua kuwa mada zinazotokana na tikitimaji ambazo ni mboga zinazopatikana sana India, China, Amerika ya Kusini na hata barani Afrika zinaweza kusaidia kuwaepusha wanawake na kansa ya matiti.
Kwa mujibu wa uchunguzi huo uliochapishwa kwenye Jarida la Utafiti wa Kansa, majimaji (extract) yanayotolewa katika tikitimaji chungu yanayojulikana kama ‘karela’ kwa lugha ya Kihindi yanaweza kupunguza kasi ya kukua kwa seli za kansa ya matiti au hata kuua kabisa seli hizo.
Ratna Ray aliyeongoza uchunguzi huo anasema kwamba, tikitimaji chungu zina uwezo wa kuzuia kensa na kuchelewesha kutokea ugonjwa huo wa saratani ya matiti. Wanasayansi wanasema kuwa, uchunguzi zaidi unapaswa kufanywa ili kuhakikisha uwezo na usalama wa tikitimaji chungu kuhusiana na suala hilo.
Ratna Ray aidha anasema kuwa, kutumia lishe asilia ni suala linalopewa umuhimu mkubwa hivi sasa na sayansi katika kuzuia ugonjwa wa saratani unaoongezeka kila siku duniani. Kwa muda mrefu tikitimaji chungu ambazo zina Vitamin C na mada ya flavonoid zimekuwa zikijulikana kutokana na kuwa pia na uwezo wa kuzuia kisukari na kupunguza kiwango cha sukari katika damu.
Utafiti mwingine unatujuza kwamba, licha ya komamanga, kutembea kunaweza kupunguza hatari ya kupata kansa ya matiti. Utafiti huo mpya uliofanywa na timu ya Jamii ya Saratani ya Marekani umeonesha kuwa, kufanya mazoezi kama vile kutembea kwa miguu, kunaweza kupunguza hatari ya kupata kansa ya matiti kwa wanawake ambao hawapati tena hedhi.
Utafiti huo umeonesha kuwa, kutembea kwa saa moja kila siku hupunguza kwa kiasi kikubwa hatari ya kupata ugonjwa huo. Timu hiyo ya watafiti iliwachunguza wanawake zaidi ya 73,000 walio na umri wa kuanzia miaka 50 hadi 74 na matokeo yameonesha kuwa, wanawake waliotembea kwa saa zisizopungua saba kwa wiki walipunguza hatari ya kupata kansa ya matiti kwa asilimia 14 ikilinganishwa na wale waliotembea kwa saa tatu au chini ya hapo.
Hali kadhalika wataalamu wanatuambia kuwa kipimo kiitwacho Mammography kinaweza kuokoa maisha ya wanawake wengi. Japokuwa kumekuwepo na mjadala mkubwa kuhusu uwezo wa kutambua ugonjwa wa kipimo kinachotumiwa kugundua kansa ya matiti, lakini utafiti umethibitsiha kwamba kipimo hicho kina faida kubwa.
Uchunguzi huo umeonesha kuwa, kipimo cha Mammography kina faida kubwa zaidi kuliko hasara zake, na kwamba kutumiwa kwake kunaokoa zaidi maisha ya wanawake yanayoweza kupotea kutokana na kansa ya matiti.
Ijapokuwa Mammography ina uwezo wa kuonyesha uvimbe (tumors), lakini pia kipimo hicho kinaweza kuonyesha uvimbe ambao hauna madhara na kuwafanya baadhi ya wanawake wapate wasiwasi na kufanyiwa operesheni bila kuwa na tatizo.
Kwa hivyo wataalamu wamewashauri wanawake wasizembee na kuwahimiza wafanyiwe kipimo hicho, kwani faida zake ni kubwa zaidi kuliko hasara. Si vibaya kujua kuwa, nchini Uingereza pekee zaidi ya wanawake 45,000 hugunduliwa kuwa na saratani ya matiti kila mwaka, na zaidi ya wanawake 12,000 hufariki dunia kutokana na ugonjwa huo.
Dk. Susan Higginbotham mmoja wa wataalamu wa ugonjwa huo nchini Marekani anasema kuwa, kula vyakula visivyokuwa na mafuta mengi, kuwa na uzito unaotakiwa kiafya, kufanya mazoezi pamoja na kuacha pombe bila kusahau kunyonyesha, kunaweza kusaidia wanawake wasipate ugonjwa wa saratani ya matiti.
Wanasayansi wanahitimisha kwa kusema kuwa, namna mtu anavyoishi ndilo suala muhimu sana linaloainisha iwapo mtu anaweza kupata ugonjwa huo au la. Kwa hivyo, tunashauriwa kufanya mazoezi kila siku kwa muda usiopungua nusu saa, huku akinamama wakishauriwa kupunguza kunywa pombe au kuacha kabisa.