The House of Favourite Newspapers

Kombe la Dunia 2022: Ufahamu Uwanja Uliojengwa kwa Makontena 974 Qatar, Kutolewa Bure Kwa Nchi Masikini

0

UWANJA huu umepewa jina la 974 ambayo ni idadi ya makontena ya kusafirishia mizigo yaliyotumika kuujenga na kuufanya kuwa uwanja wa kipekee zaidi duniani, namba 974 pia ni namba inayotumika na taifa hilo wakati kupiga simu za kimataifa.

Uwanja huu unafahamika kwa jina la Ras Abou Abood ni wakuvutia kama vilivyo viwanja vingine kwenye michuano ya Kombe la Dunia mwaka huu 2022, lakini kutokana na matakwa ya dunia ya kupunguza hewa ukaa aina hii ya ujenzi ni hatua muhimu kwa utunzaji wa mazingira.

Uwanja huu uwezo wa kubeba watu 40,000 uko umbali wa kilomita tatu mashariki kutoka mji mkuu wa Doha, shughuli za ujenzi wake zilianza mwezi Novemba mwaka 2018 na hadi kufikia mwezi Novemba mwaka 2021 ulikuwa umekamilika.

Licha ya mambo mengine shabaha ya muundo wa uwanja huu ni kuonesha utamaduni na uimara wa biashara ya usafirishaji kwa njia ya maji kwa taifa hilo.

Makontena yaliyotumika katika ujenzi wa uwanja huu yalitengenezwa nchini China na baadhi ya makontena hayo pia yalitumika kubebea vifaa vya ujenzi wa kiwanja hicho huku vyuma vilivyotumika vikitoka vietnam na uturuki.

Licha ya kutumika kama kuta za uwanja huu pia makontena hayo yanatumika kama vyumba vya huduma mbalimbali uwanjani hapo kama vile vyumba vya kubadilishia nguo kwa wachezaji, vyumba vya waamuzi, vyoo na huduma nyingine muhimu ndani ya kiwanja ikwemo ofisi za utawala.

Huu utakuwa ndio uwanja pekee kwenye michuano hii usiotumia viyoyozi na kuufanya kuwa rafiki zaidi kwa mazingira na kupunguza gharama za matumizi ya nishati na maji kwa asilimia 40.

Kwa mujibu wa Fifa katika michuano hii ya 2022 kiasi cha tani milioni 3.6 za gesi chafu zitakazo zalishwa kwenye michuano hii zitatoka kwenye ujenzi viwanja vya kudumu.

Mwenyekiti wa kamati ya maandalizi Yasir al Jamal Said anasema uwanja huu ni alama ya ubunifu na uendelevu.

Baada ya kukamilika kwa michuano hiyo mwezi Desemba mwaka huu huo ndio utakua mwisho wa uwanja huu nchini Qatar kwani utafunguliwa na kutolewa kama msaada kwa mojawapo ya mataifa yanayoendelea duniani, hii ikiwa ni sehemu ya ahadi wandaaji hao waliyoitoa mwaka 2010 wakati wakiwania nafasi ya kuwa wenyeji wa michuano hii.

Kwa pamoja viwanja vyote nane vimeligharimu taifa hilo dola za kimarekani bilioni 10 ambazo zimetolewa na serikali ya taifa hilo hii ikiwa ni sehemu ya dola bilioni 200 ambazo zimetengwa kutumika kwa ajali ya maandalizi ikiwa ni pamoja ujenzi wa miundombinu muhimu kama barabara, njia mpya za treni za umeme, vituo vya treni na huduma nyingine lukuki za kijamii ili kukidhi mahitaji wakati wa michuano hiyo.

Ukiachana na uwanja wa 974 ambao utabomolewa kabisa viwanja vingine navyo vita badilishwa matumizi ikiwa ni pamoja na kuvipunguza ukubwa ili kuendana na mahitaji ya raia wa taifa hilo kwa wakati huo.

Mara kadhaa mataifa wenyeji yamekuwa yakitumia mamilioni ya dola kuandaa viwanja ambavyo hutumika kwa majuma kadhaa wakati wa michuano hii kabla ya kusahaulika kabisa na hata wakati mwingine kugeuka magofu na kuwa hasara ya kudumu kwa mataifa hayo.

Qatar kama yalivyo mataifa mengine ya mashariki ya kati mchezo wa mpira wa miguu haupewi kipaumbele sana hivyo baada ya kumalizika kwa michuano hii wenyeji wamejipanga kugeuza kwa kiasi viwanja hivyo ili kukidhi mahitaji mengine ya taifa hilo.
Chumba cha kubadilisha nguo kilichotengenezwa na makontena

Hii inakuwa ni mara ya kwanza kwa taifa la mashariki ya kati kuandaa michuano hii mikubwa zaidi ya soka duniani.

Taifa hili lenye wakazi takribani million tatu linatarajia kupokea karibu idadi sawa na hiyo ya mashabiki wa soka kutoka kote ulimwenguni watakaofurika kwenye vinjwa hivyo kuanzia mwezi Novemba hadi Desemba utakapopigwa mchezo wa fainali.

Licha ya kusifiwa kwa kazi kubwa maandalizi lakini pia Qatar inatuhumiwa kwa ukiukwaji mkubwa haki za binadamu wakati wa ujenzi wa viwanja hivi, madai yanayohusisha mazingira duni ya kazi, ubaguzi, dhulma na maslahi duni kwa maelfu ya wafanyazi ambao sio raia wa taifa hilo.

Licha ya kukanusha tuhuma hizo lakini doa hilo litaendelea kusalia kwani wapo walio pata majeraha ya kudumu na hata wale waliopoteza maisha.

Huenda uwanja huu ukawa pia ndio uwanja uliotumiaka kwa muda mfupi zaidi duniani toka ulipokamilika mwezi Novemba mwaka 2021 na baada ya kukamilika kwa michuano ya Kombe la Dunia mwezi Desemba ndio utakuwa mwisho wake.

Leave A Reply