The House of Favourite Newspapers

Kombe la England lazuiwa Mlimani City

0

Premiership_trophy

KOMBE la Ligi Kuu England lililopo nchini kwa ziara maalum, jana Ijumaa mchana lilizuiwa kuingia katika viwanja vya Mlimani City jijini Dar, kwa kile kilichoelezwa kuwa wahusika hawakuwa wametoa taarifa.

Awali, kulikuwa na taarifa za kombe hilo kufika Mlimani City saa 5:00 asubuhi lakini baadaye ikaelezwa lingefika mahali hapo mchana saa 7:00.

Championi Jumamosi lililopewa taarifa za ujio wa kombe hilo, lilifika mahali hapo mapema asubuhi na baada ya kusubiri kwa muda, likaondoka na kurejea tena mchana.

Hata hivyo, mwandishi wa habari hii, aliuliza kwa wahusika wa Mlimani City na kujibiwa kuwa hawana taarifa za ujio wa kombe hilo. Kumbe wakati kombe likitakiwa kuwa Mlimani City saa 5:00, wahusika walibadili ratiba na kulipeleka katika kituo kimoja cha redio na runinga maeneo ya Mikocheni.

Hilo ni gundu juu ya gundu! Wakati mabingwa watetezi wa Ligi Kuu England, Chelsea, hali ikiwa tete kwenye ligi kuu msimu huu, nalo taji lao ambalo lipo nchini kwa maonyesho, limekumbana na mkosi wa aina yake, baada ya zoezi hilo la kuonyeshwa kugonga mwamba Mliman City.

Hata hivyo, ilipofika saa 7:00 mchana, msafara uliokuwa na kombe hilo uliwasili Mlimani City lakini ulizuiliwa na walinzi mlangoni hadi saa 8:49 mchana  kwa kile kilichoelezwa kuwa hakukuwa na taarifa za ujio wake.

Mmoja wa walinzi wa Mlimani City alisema hawakuwa na taarifa za ujio huo na hata uongozi wa mahali hapo nao haukuwa na maelekezo yoyote, ndiyo maana walizuia msafara huo kwa sababu za kiusalama.

Gari dogo la maofisa walioambatana na kombe hilo, liliondoka Mlimani City na kuelekea mahali kwingine ambako hakukufahamika, kwani hakuna mhusika aliyekuwa tayari kupokea simu kila walipopigiwa. Pia hawakujibu hata ujumbe mfupi.

Leave A Reply