The House of Favourite Newspapers

Kombe la SportPesa Mubashara ndani ya DStv

Mkurugenzi Mtendaji wa MultiChoice Tanzania Jacqueline Woiso akimkabidhi mpira Mkurugenzi wa Uendeshaji na Udhibiti wa SportsPesa Tarimba Abas muda mfupi baada ya kutangaza rasmi ushirika kati ya SportPesa na SuperSport ambapo SuperSport kupitia DStv itarusha mubashara michuano hiyo itakayoanza wiki ijayo hapa jijini Dar es Salaam.

 

Dar es Salaam, Tanzania – Jumanne, 15 Januari 2018 Wapenzi wa kandanda Afrika Mashariki, wanauanza mwaka huu kwa burudani ya aina yake kwa kushuhudia mubashara michuona maarufu ya Kombe la SportPesa itakayoonyeshwa ndani ya DStv kupitia SuperSport ambayo imepata idhini ya kuonyesha michuano hiyo kama mshirika rasmi.

 

Michuano hiyo itakayofanyika jijini Dar es Salaam itahusisha vigogo 8 wa soka kutoka Tanzania na Kenya na itatimua vumbi kuanzia Januari 22 hadi 27. Michuano hiyo itakuwa na mvuto wa aina yake hasa ukizingatia ukubwa na umaarufu wa timu zinazoshiriki zikiwemo watani wa jadi Simba na yanga, Mbao FC pamoja na Singida United kutoka Tanzania na vigogo wa soka Gor Mahia, AFC Leopard, Bandari FC and Kariobangi Sharks kutoka Kenya

 

Michuano hiyo itakuwa na mvuto wa aina yake kwani mbali na ukubwa, umaarufu na utani wa timu shiriki, pia kila timu itataka kutwaa kombe hili na hatimaye kupata fursa ya kucheza na moja ya timu maarufu ya soka nchini Uingereza – Everton FC.

Mkurugenzi Mtendaji wa MultiChoice Tanzania Jacqueline Woiso akizungumza na waandishi wa habari wa wakati wa kutangazwa rasmi kwa ushirika kati ya SportPesa na SuperSport ambapo SuperSport kupitia DStv itarusha mubashara michuano hiyo itakayoanza wiki ijayo hapa jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Mkurugenzi wa Uendeshaji na Udhibiti wa SportPesa Tanzania Tarimba Abas

 

Akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari wakati wa kutangaza rasmi ushirika huo kati ya SuperSport na SportPesa, Mkurugenzi Mtendaji wa MultiChoice Tanzania Jacqueline Woiso amesema kwa kuwa mshirika rasmi, SuperSport imepata idhini ya kuonyesha michuano hiyo mubashara kupitia DStv. “Tunafurahi kuujulisha umma wa watanzania kuwa hamu yao ya kushuhudia michuano hii mubashara kupitia DStv sasa imepatia jibu, sasa watashuhudia burudani hii ya aina yake tena kuanzia kifurushi cha chini kabisa cha Bomba” Alisema Jacqueline.

 

“Michezo yote itaonekana kupitia DStv SuperSport9 ambayo inapatikana katika vifurushi vyote. Tumeamua kufanya hivyo ili kuwapa watanzania fursa ya kushuhudia mashindano haya ambayo yanazidi kujipatia umaarufu kila uchao”

 

Mkurugenzi wa Utawala na Udhibiti wa SportPesa Tanzania Tarimba Abbas amesema “Tangu kuanzishwa kwa michuano hii miaka mitatu iliyopita, mashindano haya yamekua moja ya mashindano makubwa na yanayopendwa sana kote Afrika Mashariki.

 

Umaarufu huu unakuwa mkubwa zaidi hasa ukizingatia kuwa mshindi anapata fursa ya kucheza na timu maarufu ya Everton ya Uingereza. Kwa msingi huo, tumeamua kushirikiana na DStv kupitia SuperSport ili kuyawezesha mashindano haya kuonekana kwa mapana na marefu kwa  mashabiki walio sehemu mbalimbali.

 

Hili ni jambo kubwa sana kwani wachezaji wetu wataweza kuonyesha vipaji na viwango vyao na hivyo kuwatangaza kote duniani. Natoa rai kwa timu zinazoshiriki kuhakikisha zinaonyesha viwango vya juu  kabisa kwani huu ni ulingo muhimu wa kuonyesha uwezo na ujuzi wao wa soka kwa timu husika lakini pia na kwa wachezaji” alisema Tarimba.

 

Mshindi wa Kombe la SportPesa 2019 atajishindia USD 30,000 lakini cha muhimu zaidi ni fursa ya kucheza na timu ya Everton, moja ya timu maarufu kabisa za soka Uingereza. Mshindi wa pili atajinyakulia USD 10,000 wakati mshindi wa tatu atapata USD 7,500 na mshindi wa nne USD 5,000. Timu zote zitakazo tolewa robo fainali zitapata USD 2,500 kila moja.

Comments are closed.