The House of Favourite Newspapers

Kongamano la Kimataifa Ubora wa Elimu Kufanyika Dar

0
Meneja wa Program TEN/MET, Martha Makala (katikati) akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam kuhusiana na Kongamano la Tatu la Kimataifa la Ubora wa Elimu (3rd International Quality Education Conference  IQEC), linalotarajia kufanyika siku tatu mfulilizo kuanzia tarehe 27 hadi 29 Novemba 2023 Dar es Salaam. Kulia ni Afisa Mawasiliano wa Policy Forum, Richard Angelo akifuatilia

 

MTANDAO wa Elimu Tanzania (TEN/MET) unaoundwa na Asasi za Kiraia (AZAKI) 219 zinazofanya kazi katika sekta ya elimu Tanzania Bara tangu 1999 umetangaza rasmi tarehe ya kufanyika Kongamano la Tatu la Kimataifa la Ubora wa Elimu (3rd International Quality Education Conference – IQEC), linalotarajia kufanyika siku tatu mfulilizo kuanzia tarehe 27 hadi 29 Novemba 2023.

Akizungumza na vyombo vya habari mapema leo jijini Dar es Salaam, Meneja wa Program TEN/MET, Martha Makala amesema Kongamano hilo la kimataifa litafanyika Serena Hotel jijini Dar es Salaam huku likiwakutanisha pamoja wadau takribani 350 wanaotekeleza afua za kuboresha elimu kutoka sehemu mbalimbali duniani kujadili na kushirikishana mawazo, uzoefu na changamoto mbalimbali juu ya mustakabali wa elimu wakati dunia inaposhuhudia kipindi cha Mapinduzi ya Nne ya Viwanda.

 

Alisema Kongamano hilo limeandaliwa na TEN/MET kwa kushirikiana na UNICEF, School 2030, Policy Forum, Vodacom na Coalition of Good Schools, ili kutoa fursa na njia kwa watunga sera, watafiti, wasomi, wadau, wanafunzi na wadau wa maendeleo kutoka ndani na nje ya Afrika, kujadiliana na kushirikishana uzoefu wao na maarifa juu ya nafasi ya elimu ya katika kukabili mabadiliko yanayokabili ulimwengu sasa.

“Mkutano wa mwaka huu utazingatia kaulimbiu isemayo,”Kutafakari Upya Mifumo ya Elimu kukabili Mapinduzi ya Nne ya Viwanda” (Rethinking Education Systems in the 4th Industrial Revolution). Kauli mbiu hii inasisitiza umuhimu wa kufikiria upya mifumo ya elimu ili kuendana na mabadiliko makubwa yanayosababishwa na mapinduzi ya kiteknolojia. Katika mkutano huu, washiriki watapata fursa ya kujifunza kutoka kwa wataalamu wa elimu, wawakilishi wa serikali, walimu, wanafunzi, na watafiti wanaofanya kazi kuboresha mifumo ya elimu duniani kote,” alisema Meneja wa Program TEN/MET, Bi. Makala huku akiongeza tayari nchi kadhaa zimethibitisha kushiriki katika mkutano huo.

JF7A8706
Meneja wa Program TEN/MET, Martha Makala akisisitiza jambo kwenye mkutano na wanahabari kuhusiana na Kongamano la Tatu la Kimataifa la Ubora wa Elimu linalotarajia kufanyika kuanzia tarehe 27 hadi 29 Novemba 2023 Dar es Salaam. Kushoto ni Meneja wa Program wa Shule Direct, Denish Otieno.

Aidha akifafanua zaidi alizitaja mada zinazotarajiwa ni pamoja na Mikakati ya kuongeza upatikanaji wa elimu bora kwa wote, Mchango wa teknolojia katika kuboresha mifumo ya elimu, Uendelezaji wa mbinu za kufundishia na kujifunzia kwa karne ya 21, Jinsi ya kukuza stadi za kiufundi kwa ajili ya viwanda vya baadaye na Kubadilishana uzoefu ndani na nje ya Tanzania kuhusu mambo mazuri yanayofanyika kwenye sekta ya elimu.

Mada zingine zitakazowasilishwa na kujadiliwa katika kongamano ni kujadili matokeo ya utafiti kuhusu tafiti mbalimbali za elimu, Kubadilishana uzoefu kuhusu mbinu bunifu za ugharimiaji wa elimu – mitazamo ya kimataifa/ na ya ndani na Kutoa fursa kwa wadau wa elimu kuonyesha juhudi/afua/kazi zao katika sekta.

Meneja wa Program wa Shule Direct, Denish Otieno (katikati) akifafanua jambo kwa waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam kuhusiana na Kongamano la Tatu la Kimataifa la Ubora wa Elimu (3rd International Quality Education Conference  IQEC), linalotarajia kufanyika kuanzia tarehe 27 hadi 29 Novemba 2023 Dar es Salaam. Kushoto ni Meneja wa Program TEN/MET, Martha Makala na Afisa Mawasiliano wa Policy Forum, Richard Angelo (kulia).

Kila mwaka TEN/MET huandaa Mkutano wa Kongamano juu ya Elimu Bora ambapo hutoa fursa kwa wadau wa elimu ikiwepo serikali, watunga sera, vyuo vikuu, wanafunzi, waalimu, watafiti, taasisi za elimu, mashirika ya umma na binafsi, Washirika wa Maendeleo (Development Partners) pamoja na wadau mbalimbali wa elimu wa ndani na nje ya nchi kujadili hali ya ubora wa elimu inayotolewa kwa sasa ili kubadilishana mawazo na kushirikishana uzoefu kwa lengo la kuboresha utoaji wake na kuunda mustakabali bora wa utoaji elimu hapa nchini. Mkutano huu pia unalenga kuhamasisha mazungumzo na hatua stahiki za kuimarisha mifumo ya elimu inayotolewa katika nchi yetu ili kwenda sambamba na ulimwengu wa leo unaobadilika kwa haraka sana.

Kwa maoni na taarifa zaidi za namna ya kushiriki, tafadhali tembelea tovuti yetu www.tenmet.or.tz na mitandao yetu ya kijamii kupitia Instagram(@tenmet), Facebook na X (@ten_met).

Leave A Reply