The House of Favourite Newspapers

Kongamano Uchumi wa Bluu Laibua Fursa Lukuki

0
Waziri wa Uchumi wa Bluu na Uvuvi Zanzibar, Suleiman Makame akizungumza wakati wa kufunga kongamano la uchumi wa bluu lililoandaliwa na Chuo cha Bahari (DMI) na kufanyika kwenye ukumbi wa kimataifa wa Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam

 

SERIKALI imesema inaweka mazingira mazuri kuhakikisha kipaumbele kwenye fursa zilizoko kwenye uchumi wa bluu kinakuwa kwa watanzania kabla ya wageni kunyakua fursa hizo zinazopatikana kwenye bahari.

 

Hayo yalisemwa jana na Waziri wa Uchumi wa Bluu na Uvuvi Zanzibar, Suleiman Makame wakati akizungumza kwenye ufungaji wa konagamno la siku mbili la uchumi wa bluu, lililoandaliwa na Chuo cha Bahari Dar es Salaam (DMI).

Waziri wa Uchumi wa Bluu na Uvuvi Zanzibar, Suleiman Makame akimpongeza mdau wa bahari wa muda mrefu, Ibrahim Beendera wakati wa kufunga kongamano la uchumi wa bluu lililoandaliwa na Chuo cha Bahari (DMI) na kufanyika kwenye ukumbi wa kimataifa wa Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam

 

Alisema iwapo watanzania wengi watachangamkia fursa hizo na kuzitumia kwa uzalishaji fedha zitakazopatikana zitawasaidia kwa maendeleo na kubaki kwenye mzunguko wa uchumi tofauti na iwapo fursa hizo wzitachukuliwa na wageni.

 

“Kwa muda mrefu tumeona meli za uvuvi za kigeni zikivua kwenye bahari yetu zikichukua rasilimali zetu zilizopo baharini na sisi kubaki kuwa watazamaji mimi nadhani huu ni wakati wa kujipanga ili tuzitumie wenyewe kwasababu uwezo huo tunao,” alisema

Waziri wa Uchumi wa Bluu na Uvuvi Zanzibar, Suleiman Makame akiwa kwenye picha ya pamoja na wageni mbalimbali wakati wa kufunga kongamano la uchumi wa bluu.

 

Alisema kwenye bahari kuu maharamia wamekuwa wakijitokeza kwa wingi na kuchukua rasilimali za nchi hivyo hali hiyo haipaswi kuendelea na wananchi wachukua nafasi kwa kwenda kuvua bahari kuu.

 

Aliutaka uongozi wa Chuo cha Bahari (DMI) kuboresha mitaala yake na kufundisha kozi ya ubaharia wa uvuvi kwani kuna meli nyingi za uvuvi zinakuja ambazo zitahitaji wataalamu.

 

Alisema miezi mitatu iliyopita Serikali ilipokea meli ya uvuvi wa bahari kuu hivyo kuna uhitaji wa mabaharia wazalendo wa uvuvi ambao watahudumia meli hiyo na zingine zinazokuja badala ya kutegemea wataalamu wa kigeni.

 

“Mimi siyo baharia ila nimekaa sana na mabaharia ila wengi ninaowajua siyo mabaharia wa uvuvi, wengi ni manahodha wa meli, wahandisi wa meli sasa mkuu wa chuo cha DMI kwenye mitaala yako weka hii ya uvuvi wa bahari tuzalishe wataalamu wetu wenyewe,” alisema

 

Waziri alisema watanzania wengi bado hawajaitumia bahari ipasavyo kwa kuendelea kufanya uvuvi mdogo mdogo hivyo kuna haja ya kubadilika na kwenda kufanya uvuvi kwenye bahari kuu ili kuchangia kwenye ukuaji wa uchumi kwani huko ndiko wanapatikana samaki wengi.

 

“Sisi Zanzibar tumeshaanza kujipanga kwenda kwenye uvuvi wa bahari kuu sasa nanyinyi mjipange msiendelee kuwa watu wa kutoa vibali vya uvuvi kwa wageni na kubaki kuwa wasindikizaji wakati rasilimali zinazidi kuchukuliwa na wageni, tubadilike kama ytulivyobadilika kwenye madini,” alisisitiza Waziri.

 

Aliwataka washiriki kwenda kutekeleza kwa vitendo yale waliyojifunza kwenye kongamano hilo la siku mbili na kuwaelimisha watu ambao hawakupata fursa ya kuhudhuria kuhudu fursa zinazopatikana baharini.

 

“Tumekaa hapa kwa siku mbili na tumeelezwa nini maana ya uchumi wa bluu na fursa zinazopatikana baharini sasa kinachofuata ni kutekeleza kwa vitendo kuhakikisha nchi yetu inanufaika ipasavyo na bahari na vilivyomo ndani yake tusiwachie wageni,” alisema

 

Mkuu wa Chuo cha Bahari Dar es Salaam (DMI), Dk Tumaini Gurumo alisema chuo hicho kwa muda mrefu kimekuwa ikitoa mabaharia ambao siyo wa uvuvi hivyo kinaweka mazingira ya kuwafundisha mabaharia hao.

 

“Tunafahamu kwamba uendelezaji wa rasilimali watu ni muhimu sana katika kuufikisha uchumi wa bluu pale ambapo serikali inapotaka kuufikisha hivyo maagizo ya waziri tumeyapokea na tunaenda kuyatekeleza,” alisema

 

Alisema ni kweli kwa muda mrefu sasa watanzania wengi wamekuwa wakifanya uvuvi mdogo mdogo wa kujikimu usiokuwa na tija kwao hivyo kwa dhana ya sasa ya uchumi wa bluu serikali inataka wananchi wabadilike na waachane na uvuvi wa kujikimu na waende bahari kuu.

“Kuna watu wanaishi kando ya maji lakini wamezoea uvuvi wa mlo wa siku unakuta mtu amezoea akiamka asubuhi babu yangu alikuwa akiamka asubuhi anaenda kuchukua samaki kidogo hapo kusogeza maisha sasa hayo tunataka kuachana nayo twende mbali zaidi,” alisema

Aliipongeza DMI kwa kuandaa kongamano hilo alilosema limesaidia kwa kiwango kikubwa kuwaelimisha wananchi wengi ambao walikuwa hawajui maana halisi ya uchumi wa bluu na rasilimali zinazopatikana baharini.

Leave A Reply