Kopa: Nitazeeka mwili, siyo sauti

KATIKA kazi yangu hii ya kuandika na kuhoji mastaa kwa zaidi ya miaka 16, nimekutana na kumuona mara nyingi mno, mwanamama wa chuma (iron lady) ambaye ni mwimbaji mkongwe wa muziki wa Taarab ya kisasa (modern taarab), Khadija Omar Abdallah Kopa ‘Bi Khadja’.

Naunga mkono hoja kwamba, huyu ni malkia kwelikweli wa Mipasho Afrika Mashariki na Kati. Itoshe kusema Bi Khadja ni nembo ya muziki huu mtamu wenye asili ya mwambao wa Bahari ya Hindi inayopatikana Mashariki mwa Tanzania, Kenya, Somalia, Ethiopia, Sudan, Misri, Msumbiji, Zimbabwe, Afrika Kusini na visiwa vingi ndani yake.

Kwa mdomo wake, Bi Khadja aliniambia amezaliwa mwaka 1963 kisiwani Zanzibar. Ni mwenyeji wa Kijiji cha Donge kilichopo Mkoa wa Kaskazini, Unguja visiwani Zanzibar.

Katika ujana wake akiwa shule pamoja na madrasa, alikuwa anapenda mno kuimba, aliimba sana kaswida na nyimbo za aina mbalimbali katika matamasha yaliyofanyika shuleni.

Katika ujana wake, alitamani siku moja kuwa mwimbaji mashuhuri hapa duniani. Miaka ya 1990 ndoto yake ilianza kufanya kazi alipojikita kwenye muziki wa Taarab Asilia (Traditional Taarab). Alianza shughuli ya uimbaji akiwa na kikundi kikongwe cha Taarab Asilia huko Zanzibar cha Culture Musical Club.

Baada ya hapo, ndipo kipaji chake kilipoonekana na kutakiwa kujiunga na vikundi vikubwa vya Taarab vya Tanzania Bara ambavyo ni Muungano na TOT Taarab. Alipojiunga na vikundi hivyo, kulikuwa na ushindani mkubwa wa muziki wa Taarab ya mipasho kwa upande wa waimbaji kutupiana madongo. Madongo hayo mengine huwa ni ya kweli na mengine huimbwa ili kuiburudisha jamii.

Hali hiyo ilimfanya aitwe Malkia wa Mipasho Afrika Mashariki na Kati kutokana na nyimbo zake kuwa ndizo zinazoongoza kupasha na kutoa madongo halisi kwa walengwa.

Katika shughuli zake za uimbaji, alitamani mno kazi yake ije kurithiwa na wanawe ambao ni Omary Kopa na Mohammed Mbwana. Omar ni mtoto wa kwanza wa Bi Khadja, lakini kwa bahati mbaya alifariki dunia mwezi Machi, 2007. Kupitia Taarab, Bi Khadja ameshatwaa tuzo nyingi zikiwemo zile maarufu za

KTMA (Kilimanjaro Tanzania Music Awards). Pia ametajwa kushiriki Tuzo za AFRIMMA akiwa ni mwanamuziki pekee wa Taarab aliyeshiriki tuzo hizo katika kipengele cha Mwanamke Bora Afrika Mashariki na Kati (Best Female in East Central Africa).

Mbali na kufanya kazi na TOT, pia Bi Khadja anamiliki bendi yake mwenyewe aliyoipa jina la OGOPA KOPA CLASSIC BAND.

Huyu ndiye Malkia wa Mipasho Afrika Mashariki na Kati. Baadhi ya nyimbo zake zilizoshika vilivyo ni pamoja na Y2K (Manjonjo), Gendaeka, Mwanamke Mambo Makalio Majaaliwa, Gwinji Atambe Ana Nini, Kubali Matokeo Bwana Hatakutafuta, Utaishia Kunawa Hatuli Sahani Moja, Top in Town, Lady With Confidence, Zee la Nyeti

Unaringa Ushapima Wewe?, Fahari ya Mwanamke, Mama Mkubwa na nyingine nyingi.

UWAZI SHOWBIZ imefanya mahojiano maalum na Bi Khadja ambapo anafunguka juu ya mambo mbalimbali ikiwemo suala la kuzeeka mwili, lakini siyo sauti na suala la mwanawe, Zuchu kusainiwa kwenye Lebo ya Wasafi.

UWAZI SHOWBIZ: Hongera Bi Khadja kwa heshima kubwa uliyonayo kwenye muziki wa Taarab, nini siri yako?

KOPA: Siri kubwa ni kujua unafanya nini, kutengeneza vitu vizuri ambavyo hasa mashabiki wanavipenda. Kingine kikubwa ni kujiheshimu mwenyewe kabla hujaheshimiwa.

UWAZI SHOWBIZ: Wanamuziki wengi wana tabia ya kuhama bendi mbalimbali, wewe umewezaje kudumu bendi moja ya TOT kwa zaidi ya miaka 30?

KOPA: Kwanza kuhama bendi kila wakati ni kujishushia heshima yako na mara nyingi unaua kipaji chako. Mimi sikuwa na sababu ya kuhama maana kama nataka kuonesha ujuzi, naonesha kwenye bendi yangu na tena sitakwenda popote, nitafia hapahapa (TOT).

UWAZI SHOWBIZ: Baada ya kufariki dunia kwa Kiongozi wa Bendi ya TOT, John Komba ambaye pia alikuwa Mbunge wa Mbinga- Magharibi, bendi imeyumba siyo kama zamani, wewe unalichukuliaje hilo?

KOPA: Ni kweli bendi haiko kama alivyokuwepo mwenyewe, lakini kama baba akifariki dunia ndiyo uihame nyumba? Ni kwamba kama una uwezo, unaboresha na ndivyo ilivyokuwa kwangu.

UWAZI SHOWBIZ: Kipindi cha nyuma maonesho ya Taarab yalikuwa yanajaza sana tofauti na sasa, nini mtazamo wako?

KOPA: Hilo ni kweli kabisa, mengi sana yamefanya muziki huu kuyumba mpaka kuna wakati unaona uvivu wa kutunga nyimbo nyingine. Zamani mtu anasubiria kabisa Khadija Kopa atatoa kijembe gani na marehemu Nasma Kidogo atasemaje, lakini sasa hivi hakuna kitu kama hicho.

UWAZI SHOWBIZ: Kutokana na kubadilika kwa muziki huu, unaendeshaje maisha yako kwa sasa?

KOPA: Mimi sina taabu kabisa, nafanya kazi ya ushereheshaji kwenye sherehe mbalimbali. Pia ninaimba kwa mtu akinialika mpaka nje ya nchi. Si haba, ninapata chochote cha kulea familia yangu.

UWAZI SHOWBIZ: Mara nyingi sasa hivi Taarab wanapopiga kiingilio kinakuwa ni kinywaji, mmeshawahi kufanya hivyo kwenye bendi yenu?

KOPA: Asilani siwezi kwenda kuimba kwa kiingilio cha bia. Bora nikae sina kitu, lakini siwezi kufanya hivyo, kwangu ni marufuku kabisa.

UWAZI SHOWBIZ: Kipindi cha nyuma ulisema kuolewa ni stara, sasa tangu mumeo amefariki dunia, una mpango gani?

KOPA: Bado hajatokea wa kunipa stara, akitokea nitaolewa maana ni vyema kuolewa kuliko kutenda dhambi.

UWAZI SHOWBIZ: Ni takriban miaka 30 unafanya kazi ya kuimba, nini mafanikio yako?

KOPA: Mafanikio yapo kwa kweli, nimeweza kujenga, kusomesha watoto wangu mpaka wajukuu. Nina usafiri, hilo namshukuru sana Mungu.

UWAZI SHOWBIZ: Zuchu amekuwa maarufu mno baada ya kusainiwa kwenye Lebo ya WCB, unamzungumziaje Zuchu?

KOPA: Kwanza kabisa nataka kuwaambia watu siku zote, subira huvuta heri kwa sababu Zuchu ameimba muda mrefu sana. Kwa uweza wa Mungu sasa ndiyo ameanza kuwika. Ninachokijua kwa Zuchu ni mvumilivu sana na subira yake imemfikisha hapo alipo.

UWAZI SHOWBIZ: Kuna maneno mengi mno yanasemwa kutokana na hivi sasa anang’aa zaidi kuliko hata wanawake wengine wa Bongo Fleva kwamba ana uhusiano na Mkurugenzi wa WCB, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’, hili unalizungumziaje?

KOPA: Siwezi kuwakataza watu kusema, hiyo ni hulka ipo siku zote, lakini wakati hana mafanikio, alikuwa hazungumziwi kwa baya au zuri, sasa hivi wanaona ameanza kuonesha kipaji wanaleta maneno. Siwezi kuwazuia, mimi kama mama, nitasimamia maadili ya mtoto wangu ipasavyo.

UWAZI SHOWBIZ: Vipi kuhusu Corona, imekuathiri vipi kwenya kazi zako, ukiangalia ni mwanamuziki na kumbi nyingi zilifungwa?

KOPA: Yaani nimeteseka sana kwa kweli, hakuna pesa, kuna wakati unatamani kabisa kuacha kazi ya kuimba, maana hali ilikuwa mbaya sana. Bora sasa hivi, ila mambo yatakaa sawa.

UWAZI SHOWBIZ: Kwa faida ya msomaji, uliingiaje kwenye kuimba Taarab na siyo muziki wa aina mwingine?

KOPA: Unajua mimi nilianza kuimba muziki huu wa mwambao tangu 1990 na bendi ya kwanza kujiunga nayo ilikuwa Culture Musical Club. Kisa cha kujiunga bendi hiyo ni kwamba, siku moja nilikuwa nimekaa nje najiimbia tu wimbo, mara akapita babu yangu aliyekuwa akifanyia kazi kwenye kundi hilo kule Zanzibar, akanisifia ya kwamba najua kuimba vizuri sana, basi akachukua hatua ya kuandika barua kwa niaba yake bila kumshauri, akaipeleka Culture Musical Club kuomba nijiunge nao mpaka TOT walivyonisikia na kuja kunichukua.

UWAZI SHOWBIZ: Nakushukuru sana kwa ushirikiano wako Bi Khadja.

KOPA: Asante sana.

Toa comment