
Mar 04, 2025 07:43 UTC, Korea Kaskazini yalaani uchokozi wa kijeshi wa Marekani
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Korea (DPRK) imelaani vikali uchokozi wa kisiasa na kijeshi wa Marekani baada ya meli ya kubeba ndege za kivita ya Jeshi la Wanamaji la Marekani kutia nanga katika bandari ya Busan, Korea Kusini.
Kauli hiyo imetolewa kupitia tamko rasmi la Kim Yo Jong, dada wa kiongozi wa DPRK, Kim Jong Un. Tamko hilo lilichapishwa Jumanne na Shirika la Habari la Korea Kaskazini (KCNA).
Tamko lake limesema:”Mara tu baada ya utawala mpya wa Marekani kuingia madarakani mwaka huu, umeongeza uchokozi wa kisiasa na kijeshi dhidi ya DPRK, ukiendeleza sera ya uhasama ya utawala uliopita.”
Alimtuhumu Rais wa Marekani wa zamani, Donald Trump, kwa kushadidisha uchokozi wa kisiasa na kijeshi dhidi ya nchi yake.
Bi. Kim ameongeza kuwa utawala mpya wa Marekani unaendeleza sera hiyo hiyo ya uhasama dhidi ya Pyongyang.
Aliangazia kuwa Marekani imeongeza mvutano wake na Pyongyang mwezi huu kwa kuleta meli ya kubeba ndege za kivita, USS Carl Vinson, katika bandari ya Busan.
Kwa mujibu wa taarifa ya Jeshi la Wanamaji la Marekani, manowari ya USS Carl Vinson, ambayo ni meli kuu ya kundi la mashambulizi la Marekani, iliwasili Busan Jumapili.
Mafunzo ya pamoja ya kijeshi kati ya Korea Kusini na Marekani yanayojulikana kama “Freedom Shield” yanatarajiwa kuanza mwezi huu.
Mazoezi ya kijeshi yanayorudiwa mara kwa mara kati ya Korea Kusini na Marekani yameilazimu Korea Kaskazini kulazimika kuendeleza teknolojia yake ya silaya za nyuklia na makombora.
Pyongyang inaona mazoezi hayo ya kijeshi ya pamoja kama maandalizi ya uvamizi dhidi yake.
Mahusiano kati ya Korea Kusini na Korea Kaskazini yako katika hali mbaya zaidi kwa miaka mingi, huku Korea Kaskazini ikifanya majaribio mengi ya makombora ya balistiki mwaka jana kama njia ya kupinga mazoezi ya kijeshi ya pamoja ya Marekani na Korea Kusini.
Wiki iliyopita, Korea Kaskazini ilifanya jaribio la kurusha makombora ya kimkakati ya cruise katika Bahari ya Njano, ikiwa ni sehemu ya mazoezi ambayo Pyongyang ilisema yalilenga kuonyesha uwezo wake wa “mashambulizi ya kujibu”.