The House of Favourite Newspapers

KOREA KUSINI, KASKAZINI KUZUNGUMZIA OLIMPIKI YA 2018

KOREA ya Kusini imependekeza kuweko mazungumzo na Korea ya Kaskazini, Januari 9 mwaka huu, kuhusu uwezekano wa nchi hiyo ya kaskazini kushiriki Michezo ya Olimpiki ya Majira ya Baridi itakayofanyika mwaka huu (2018).

Kwa mujibu wa shirika la habari la BBC la Uingereza, hatua hiyo inatokana na kauli ya kiongozi wa Kaskazini, Kim Jong-un, kwamba anafikiria kupeleka timu kwenye michezo hiyo itakayofanyika jijini Pyeongchang, Korea Kusini, mwezi Februari.

Kiongozi huyo alisema ili kufikia mwafaka, pande hizo mbili zilihitajika kukutana ili kulijadili suala hilo kwani litakuwa moja ya kuimarisha uhusiano wao ambao umezidi kuwa wa wasiwasi.

Waziri wa Korea Kusini anayeshughulikia masuala ya kuziunganisha nchi hizo mbili, Cho Myoung-gyon, alipendekeza leo kamba wawakilishi wa nchi hizo wakutane Panmunjom, sehemu inayojulikana kama “kijiji cha amani”.

“Tunatarajia kwamba Kusini na Kaskazini zitakutana na kujadili ushiriki wa Kaskazini katika Michezo ya Pyeongchang na masuala mengine yatakayoimarisha uhusiano wa nchi hizi,” alisema Cho.

Haijafahamika ni watu gani watakaoshiriki mazungumzo hayo, kwani Kaskazini bado hawajatoa kauli yoyote kuhusu suala hilo.

Mazungumzo ya mwisho ya ngazi za juu kati ya nchi hizo yalifanyika Desemba 2015 katika eneo la viwanda la Kaesong ambapo yalimalizika bila ya taarifa yoyote.

IMEFASIRIWA NA WALUSANGA NDAKI

Comments are closed.