KOROSHO ni muhimu sana katika mwili wa binadamu. Kwa Tanzania zao hili hulimwa kwa wingi katika mikoa ya pwani hasa Mtwara, Lindi na Pwani. Wengi wetu hatuli korosho na hata pale tunapokula, hula kama kitafunwa cha kuchangamsha mdomo tu, na wala siyo kitu muhimu sana kuliwa. Korosho ina faida nyingi sana kiafya, hasa katika magonjwa yenye uhusiano na magonjwa ya moyo, kama ambavyo tutaweza kuona katika makala ya leo.
Siyo tu kwamba korosho zina kiwango kidogo cha mafuta lakini pia zina aina ya mafuta ambayo hutoa kinga kwenye moyo. Aidha, ndani ya korosho, kuna kirutubisho aina ya Oleic Acid ambacho huimarisha afya njema ya moyo na huwafaa hata wagonjwa wa kisukari.
Utafiti wa hivi karibuni uliochapishwa kwenye jarida la masuala ya virutubisho nchini Uingereza liitwalo British Journal of Nutrition, umeonesha kuwa watu waliopendelea kula korosho na bidhaa zake, kama butter, idadi ya vifo vitokanavyo na ugonjwa wa moyo vilipungua kati ya asilimia 11 na 19.
Watu wanaotumia korosho angalau mara nne kwa wiki, walionesha kuondokewa na hatari ya kupatwa na ugonjwa wa moyo kwa asilimia 37. Inashauriwa kutafuta korosho kiganja kimoja au kijiko kimoja cha chakula kilicho jaa ‘nut butter’, kula hivyo mara nne kwa wiki.
Korosho pia ni chanzo kizuri cha madini aina ya copper ambayo ni muhimu sana katika mwili wa binadamu, korosho pia ina madini yanayoimarisha mifupa na kinga ya mwili. Watu wanaopenda kula korosho, angalau mara mbili kwa wiki, hakuna uwezekano wa kuongezeka uzito na badala yake wanaweza kupungua.
Hivyo inashauriwa kupenda kula korosho au butter kwa afya yako na wala hakuna haja ya kuhofia kuongezeka uzito. Kisayansi inashauriwa kutumia korosho kiasi, kwani ina virutubisho muhimu na adimu, ambapo tafiti zilizofanyika zimebainisha kuwa mtu anayetumia korosho hufaidika kwa kuongeza vitu vifuatavyo mwilini.
Ina miliki calories 155, ni vyakula vinavyohitajika mwilini ili kutengeneza nguvu na kuupa mwili virutubisho vyote vinavyotakiwa katika kujenga mwili, ina miliki gram 9.2 za kabohaidreti, gram 5.2 za Protini na Vitamini E, B6 pamoja na gram 9.5 za vitamini K, gram 10 za madini ya Calcium, mbali na madini hayo ina umiliki mkubwa wa madini ya Zinki, Magneziam, Potasiam, kopa, na Asidi ya Folik.
Hivyo katika mwili wa binadamu korosho husaidia mambo yafuatayo: Inasaidia kunyonya mafuta katika mwili wa binadamu hivyo huulinda mwili dhidi ya magonjwa ya moyo kama tulivyoona hapo juu na kuusaidia moyo kuwa wenye afya njema. Kula korosho mara kwa mara husaidia mwili kuwa na madini ya chuma ambapo ugonjwa wa Anemia hutokana na upungufu wa madini ya chuma hivyo ulaji wa Korosho hukinga mwili na magonjwa ya damu ikiwemo Anemia.
Korosho husaidia uwezo wa macho kuona kama ilivyo kwa karoti. Korosho inamiliki kirutubisho kisayansi kijulikanacho kwa jina la Zea Xanthin ambacho huilinda retina ya jicho dhidi ya miale na uchafu ambao unaweza kudhuru jicho. Korosho ni nzuri kwa kutunza ngozi, kutokana na virutubisho na madini kwa kung’arisha ngozi, kama Zinki, Magnesium, Fosforas na chuma lakini pia uwepo wa madini ya selenium ambayo hulinda ngozi dhidi ya magonjwa ya kansa.
Comments are closed.