Kilichoonekana Kwenye Video ya Ushahidi Kesi ya Mbowe

VIDEO ya Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Freeman Mbowe na wenzake, iliyoibua mvutano katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam hatimaye imeonyeshwa leo tarehe 19 Agosti 2019.

 

Kwenye video hiyo, Mbowe anaonekana akiwaambia wafuasi waliokuwa kwenye mkutano wa kampeni wa kumnadi Salum Mwalimu, aliyekuwa mgombea kwenye uchaguzi mdogo wa jimbo la Kinondoni, waende kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Kinondoni.

 

Katika kesi hiyo namba 112/2018, shahidi namba sita – Koplo Charles – wa upande wa Jamhuri ndiye aliyewasilisha ushahidi wa video hiyo, ukilenga kuithibitishia mahakama, kwamba Mbowe na wenzake walifanya uchochezi kwenye shitaka hilo.

 

Ushahidi huo wa video ulionyeshwa mahakamani hapo kwa kutumia ‘projector’ baada ya Hakimu Mkazi, Thomas Simba kutoa uamuzi katika maombi ya upande wa Jamhuri ya kutaka ushahidi huo kutumiwa mahakamani hapo.

 

Katika uamuzi wa ombi hilo, Hakimu Simba alitoa dakika 40 kwa ajili ya video hiyo kuonyeshwa kwa kutumia vifaa vya nje (external device).

 

Kwenye zoezi hilo, Koplo Charles alisaidiwa na mtaalamu wa teknolojia ya habari na mawasiliano (IT), Nazari Moshi, kutoka Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuunganisha kamera yake na vifaa vya nje vya mahakama hiyo kwa ajili ya kuonyesha video hiyo aliyoigawa mara mbili (Min div 1 &2).

 

Koplo Carles alionesha video ya kwanza aliyoipa jina la ‘Mkutano wa Chadema wa mwaka 2018’ ambayo ilionyesha baadhi ya  viongozi na wabunge wa Chadema wakiongozwa na  Mbowe, Mwenyekiti Chadema – Taifa na  Dk. Vincent Mashinji, Katibu Mkuu wa chama hicho, wakimnadi Mwalimu kwenye uchaguzi huo wa marudio.

 

Video ya kwanza yenye dakika 56 na sekunde 37, ilionyesha wabunge kadhaa wa Chadema akiwemo, John Heche (Tarime Mjini), Cecil Mwambe (Ndanda), Halima Mdee (Kawe), Ester Bulaya (Bunda Mjini), Mchungaji Peter Msigwa (Iringa Mjini) wakitoa hotuba zao za kumnadi Mwalimu.

 

Baadaye, video hiyo ilimuonyesha Mbowe akihutubia wananchi waliohudhuria katika mkutano huo na kisha kumkaribisha Mwalimu kwa ajili ya kunadi sera zake. Video hiyo iliishia hapo.

 

Video ya pili; yenye urefu wa dakika 25 na sekunde 55, iliyomuonyesha Mbowe akihutubia kisha kuwataka wananchi kuelekea ofisi ya msimamizi wa uchaguzi Wilaya ya Kinondoni.

 

Baada ya ushahidi huo wa video kumalizika, Hakimu Simba ameiahirisha kesi hiyo kwa dakika 30, na kupanga kumalizia usikilizwaji wa shahidi namba sita ambaye ni Koplo Charles katika chumba cha mahakama hiyo namba moja.


Loading...

Toa comment