Kova Amtafutia Mkude Mwanasaikolojia

KAMATI ya Nidhamu na Maadili ya Simba, ambayo ipo chini ya Mwenyekiti wake Seleiman Kova, imelazimika kusitisha adhabu ya makosa ya utovu wa nidhamu yaliyofanywa na kiungo wa timu hiyo Jonas Mkude na kuamua kumtafutia mwanasaikolojia.

 

Kamati hiyo ya Kova, ilianza kusikiliza shauri la Mkude tangu Jumamosi iliyopita sakata ambalo limechukua takribani siku nne hadi walipoazimia kuachana nalo juzi Jumatatu, huku Mkude akiendelea kuwa nje ya timu yake hadi ufumbuzi upatikane.

 

Championi Jumatano, lilizungumza na Kova ambaye aliweka wazi kwamba, wamelazimika kusitisha hukumu ya makosa yaliyofanywa na Mkude, baada ya kuangalia taratibu zinazofanywa na baadhi ya timu kubwa za nje pale mchezaji anapokutwa na matukio ya mara kwa mara kama hayo.

 

“Kamati yetu, baada ya kukaa kwa takribani siku nne, imemkuta Mkude, ana makosa ambayo yamekuwa yakijirudia mara kwa mara jambo ambalo limetulazimisha kujifunza kwa wenzetu namna ya kuchukua hatua, hivyo kwa pamoja tumeazimia kumtafutia mwanasaikolojia ili aweze kukaa naye na kujua kinachomsibu zaidi.

 

Hatua hii tumeichukua kwa kuzingatia ukubwa wa makosa yake ambayo huku nyuma ameonekana kuyafanya na kujirudia sana hivyo kwa ukubwa wa timu yetu tumeona ni vyema tusubirie majibu ya mwanasaikolojia halafu ndiyo tutatoa adhabu kwa kushirikiana naye,” alisema Kova

STORI; MUSA MATEJA ,Dar es Salaam


Toa comment