Kuelekea London Dabi… Mourinho Aikejeli Arsenal
BOSI wa Tottenham, Jose Mourinho amesema kwa sasa haangalii chini bali anaangalia juu kwani wapinzani wake Arsenal wapo chini akiwa amepishana nao pointi saba.
Tottenham itakuwa ugenini ikivaana na Arsenal kwenye Uwanja wa Emirates, leo Jumapili ikiwa ni katika kusaka pointi tatu muhimu kwenye North London Derby.
Awali mchezo ambao ulizikutanisha timu hizo, Tottenham ilishinda kwa mabao 2-0 na sasa, Spurs wapo nafasi ya saba na pointi 45 na Arsenal wana pointi 38 wakiwa nafasi ya 10.
Mourinho amesema katika mchezo huo anaona timu yake inaondoka na ushindi na kupishana na Arsenal kwa pointi 10 baada ya mchezo huu.
Kocha huyo alisema: “Naangalia juu, siangalii chini. Kama Arsenal wangekuwa wametuzidi pointi saba juu yetu ningewaangalia, lakini sasa tumewazidi kwa pointi saba ambazo ni nyingi ndiyo maana sitaki kuangalia chini.“Lakini pia tunaangalia mechi yetu inaweza kuwa sio Arsenal naangalia Aston Villa au Newcastle kwa maana hiyo tutacheza kwa nguvu hiyohiyo.
“Hata hivyo wapinzani wetu Arsenal nawaheshimu sana kwa kuwa ni klabu kubwa ambayo inahistoria kwenye soka kama sisi na wao wanajaribu kujijenga.”Kwa upande wa kocha wa Arsenal, Mikel Arteta amekiri kutishwa na safu ya ushambuliaji ya kikosi hicho.
“Tottenham ni bora hasa eneo la mbele kutokana na aina ya wachezaji ambao wanao hivyo safu yangu ya ulinzi inatakiwa kuwa makini wakutana na mastraika ambao ni tishio Ulaya kwa sasa.”Wakati Arsenal ikicheza dhidi ya Tottehman leo, michezo mingine ni Leicester v Sheffield, Southampton v Brighton na Man United v West Ham.