The House of Favourite Newspapers

Kuelekea Mashindano ya Sanaa na Utamaduni ya Mkuu wa Majeshi Tambo Zimeanza

0
Wana anga anga kazini kwenye maandalizi ya mashindano hayo.

Dar-es-Salaam Katika kuelekea mashindano ya utamaduni ya Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi nchini, Jenerali Jacob Mkunda yanayoshirikisha vikundi vya majeshi ya ulinzi hapa nchini, leo wanahabari walitembelea makambi ya wasanii wanaoshiriki mashindano hayo na kujionea tambo mbalimbali.

Tambo hizo zilikuwa zikihusisha mashindano hayo yanayotarajiwa kuanza kutimua vumbi Agosti 19 mpaka 30 mwaka huu kwenye Msasani Beach Club jijini Dar.

Kikundi cha ngoma za utamaduni Mbweni JKT kikijifua kuelekea mashindano hayo.

 

Ziara ya wanahabari ilianzia kwenye shule ya muziki ya kijeshi, iliyopo kambi ya Lugalo yalipo Makao Makuu ya Bendi ya Mwenge Jazz ambao kwa upande wao kupitia kiongozi msaidizi wa bendi hiyo, Salumu Dialo wamejitamba kuibuka na ushindi wa kwanza.

 

Dialo alijitamba kuwa wao wamejinoa vyema kabisa kwasababu wao ndio bendi mama wengine wakajipange kwanza.

Kwa upande wa ngoma za asili kambini hapo kikundi chao kiitwacho Sauti ya Umoja (JWTZ) kupitia Sajenti Ameltha Komba amesema kuwa wamejiandaa vya kutosha.

Mwenye Jazz almaarufu Wana Paselepa nao wakijifua kuelekea mashindano hayo.

Sajenti huyo amesema wanaotaka kushindana nao wajipange kwa sababu wao tangu yalipotangazwa mashindano hayo kwao ni mazoezi kuanzia asubuhi mpaka jioni.

Pamoja na tambo za maneno vikundi hivyo viwili vya kambini hapo vilipiga bonge la shoo ya kuwaonesha vionjo wanahabari waliofika kuwatembelea.

Kikundi cha utamaduni cha JKT Mgulani kikiwa kwenye mazoezi makali ya kunyakua ubingwa.

Ziara hiyo haikuishia hapo ilielekea Mbweni JKT na kuikuta bendi ya Mbweni Jazz bend ‘Wazee wa Jodari’ ambayo kabla ya kumwaga tambo za maneno waliwakaribisha wanahabari kwa bonge la shoo.

Baada ya shoo hiyo mmoja wa wasanii wa bendi hiyo aliyejitambulisha kwa jina la Rachel Chusi aliahidi bendi hiyo kukosa mpinzani kwenye mashindano hayo.

Rachel alizidi kutamba;

“Yaani kwanza tunashukuru haya mashindano kuanzishwa huu ni muda sasa wa kuonesha umahiri wetu na kuchukua ushindi mbele ya watakaojaribu kushindana na sisi. ” Alimaliza kusema Rachel.

Na kwa upande wa Bendi ya Kamandi la Anga wao kupitia msanii Jacob Sipak amesema kwa jinsi wanavyojifua ushindi lazima uende kwao wengine watakuwa wasindikizaji tu.

“Yaani ushindi ni wetu kabisa huu tunawapa taarifa tu hivyo vikundi vingine kuwa waje watusindikize tu lakini kwao wasahau labda wajaribu siku nyingine.

Ziara hiyo iliishia Kambi ya JKT Mgulani ambapo ndipo yalipo Makao Makuu ya bendi maarufu ya Kimbunga Jazz ambapo aliyeachiwa nafasi ya kumwaga tambo alikuwa ni Koplo Prexlda  Msola aliyesema kwa kutumia ukongwe wao na uzoefu wao wa muda mrefu wanaamini hakuna wa kuwasumbua.

“Hakuna asiyeijua JKT Mgulani kuwa ndio bingwa wa masuala ya sanaa na hata hao wanaotaka kushindana nasi hilo wanalitambua kabisa kuwa sisi ndiyo mabingwa.

Mashindano hayo yanatarajiwa kufanyika Msasani Beach Club kuanzia Agosti 19 mpaka 30 mwaka huu, kuanzia saa nane mchana ambapo mgeni rasmi kwenye uzinduzi huo anatarajiwa kuwa Waziri wa Sanaa, Utamaduni na Michezo Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro (Mb) na kufungwa na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mh. Dk. Stergomena Lawrence Tax (Mb). Hukuna kiingilio kwenye mashindano hayo wananchi wote wanakaribishwa kwenda kujionea burudani hizo. HABARI: RICHARD BUKOS NA NEEMA ADRIAN/ GLOBAL PUBLISHERS  

Leave A Reply