JESHI la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam limesema limejipanga vyema kuimarisha ulinzi katika kipindi cha sikukuu ya Pasaka ili kuepusha usumbufu wowote unaoweza kujitokeza na kuhakikisha wananchi wote wa jiji hilo wanasherekea sikukuu hii kwa amani na utulivu.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar, leo Machi 30, 2018, Kamanda Mambosasa amesema kuwa jeshi hilo halitamvumilia mtu yeyote atakayeleta vurugu kwa kuwa mara nyingi katika kipindi cha sikukuu watu wenye nia mbaya hutumia nafasi hiyo kufanya uhalifu ili kujipatia kipato.
“Jeshi la Polisi litahakikisha wananchi wa Mkoa wa Dar wanasherehekea Pasaka kwa amani na utulivu. Uzoefu unaonesha kwamba mara nyingi katika sherehe kama hizi watu wenye nia ovu wanajiandaa kufanya vitendo vya kihalifu ikiwa na pamoja na kufanya ujambazi ili kujipatia vipato kwa ajili ya kusherehekea sikukuu.
“Kwenye maeneo ya starehe, niwatake wananchi kuwa waangalifu, wasinywe vileo kupita kiasi ili kujiepusha na vitendo vya kihalifu.Watakaokwenda kwenye fukwe za bahari wanatakiwa wawe waangalifu na kuchukua tahadhari kubwa, wasiruhusu watoto kuogelea peke yao badala yake wawe chini ya uangalizi wa watu wazima.
“Tumejipanga vizuri kuhakikisha hakuna mtu yeyote atakayeweza kupata nafasi ya kufanya lolote katika uvunjifu wa amani, tumeimarisha doria na tunaendelea na misako maeneo yote ya jiji la Dar es Salaam katika mikoa yote mitatu na wilaya zote kumi na moja za kipolisi,” alisema Mambosasa.
Comments are closed.