The House of Favourite Newspapers

‘Kuendesha gari baada ya kunywa pombe si makosa Kenya’

 

MAHAKAMA moja ya Kiambu nchini Kenya imetoa uamuzi wa kipekee ikisema kuendesha gari baada ya kunywa pombe si makosa iwapo dereva huyo amelidhibiti vya kutosha gari analoendesha.

 

Kulingana na mtandao wa runinga ya Citizen nchini Kenya, hakimu mkazi wa Kiambu, Bryan Khaemba, alitoa uamuzi huo katika kesi ambapo dereva Michael Ngobe Mugo ameshtakiwa kwa makosa ya kuendesha gari chini ya shinikizo la pombe.

 

Mahakama hiyo iliamuru kwamba kwa dereva ambaye anaendesha gari akiwa mlevi na kupatikana na makosa, ni sharti mwendesha mashtaka awe na ushahidi wa kutosha kwamba dereva huyo alishindwa kulidhibiti gari hilo.

 

Mugo alishtakiwa kwamba mnamo tarehe 23 mwezi Mei 2018 akiwa anaendesha gari katika barabara ya Banana-Ruaka mjini Kiambu, aliendesha gari hilo akiwa mlevi na hakuwa na udhibiti mzuri wa gari lake.

 

Kulingana na mtandao huo ofisa mmoja wa trafiki ambaye alitoa ushahidi katika kesi hiyo, mshtakiwa huyo aliwashinda nguvu yeye na wenzake wawili hivyo wakashindwa kumkamata.

 

”Hilo haliwezekani kwa mtu ambaye anadaiwa kuwa mlevu chakari, ” ulisema uamuzi huo.

 

Huku akifutilia mbali kesi hiyo, mahakama hiyo ilisema kuwa mshtakiwa hakuathiriwa na pombe hiyo, sababu iliyowafanya maofisa hao kushindwa kumkamata.

 

”Naamuru kwamba upande wa mashtaka ulishindwa kuwakilisha kesi yenye ushahidi mzuri dhidi ya mshukiwa kwa kushindwa kutoa ushahidi kwamba alishindwa kulidhibiti gari alilokuwa akiendesha,”  alisema hakimu mkuu mkazi, Khaemba.

 

Mahakama iliongezea kwamba kuendesha gari chini ya shinikizo la pombe si makosa.

JIUNGE NA FAMILIA YA GLOBAL TV UPANDE MTANDAO WA MAFANIKIO

Bofya hapa kujiunga na familia ya Global TV Club ==> Global TV Family Club

 

Comments are closed.