KUFURU! BWA’MDOGO ANAYEDAIWA KUIPIGA MABILIONI SERIKALI YA JPM

UKISIKIA kuna bwa’mdogo wa miaka 34, tena anaishi Kongowe, Mbagala jijini Dar es Salaam, amefikishwa mahakamani akidaiwa kuipiga serikali ya Rais John Pombe Magufuli ‘JPM’, kiasi cha shilingi bilioni 188 habari hiyo usiichukulie poa, Uwazi linakuambia.  

 

Takribani siku tano tangu kijana huyo, Mustapha Kambangwa afikishwe Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwa tuhuma hizo, mitaani watu wengi wanafikiria kuhusu hayo mabilioni ya fedha, mambo ya kesi yake yaweke kando. Kwanza unaijua bilioni moja au unaisikia, umewahi kuishika mkononi au kuiona kwenye mkoba wa mjomba wako?

 

Kama bado hicho ni kiasi kikubwa cha fedha kwa maisha ya Kibongo kwenye usawa huu wa kuungaunga. Kama hujui bilioni moja ni sawa na mafungu 1,000 ya shilingi milioni mojamoja; hapo hakuna ubishi. Kwa msingi huo ukisikia mahali popote kuna mtu ana bilioni 188 muogope; kwa maana ukipewa kiasi hicho cha fedha matumizi yake ni kufuru.

UNAWEZA KUNUNUA NDEGE

Kwa mujibu wa mitandao, thamani ya ndege yenye uwezo wa kubeba abiria 50-60 kama Bombardier inakadiriwa kuwa ni shilingi bilioni 66. Kwa hiyo katika kiasi cha fedha kinachotajwa kuwa ni bilioni 188 ukinunua ndege yako ya thamani hiyo utakuwa umebakiza shilingi bilioni 122 kibindoni.

KUNUNUA MAGARI YA KIFAHARI

Ukiamua kujikusanyia magari ya kifahari kama Toyota V8 wanayotembelea mawaziri yanayotajwa kuwa na thamani ya shilingi milioni ya 200, kwenye bilioni moja utapata matano yenye rangi tofautitofauti huku salio lako likisoma bilioni 121.

 

Roho ikipenda kuwa na magari matata ya kisasa kama Lamborghini Huracan LP 580-2 toleo la 2018 linalouzwa dola 204 sawa na shilingi milioni 470 utapata mawili kwa shilingi milioni 938 kwenye bilioni chenji inarudi na salio lako kusoma bilioni 120. Ukitaka mabasi ya Yutong unaweza kutenga bilioni 2 na ukajipatia kumi na salio likabaki bilioni 118.

UNAWEZA KUJENGA MAGHOROFA

Ikumbukwe kwamba bilioni 188 siyo fedha ya kitoto, mzigo bado unadai pamoja na kufanya kufuru zote hizo, sasa hata ukiamua kujenga maghorofa matano ya kisasa yenye thamani ya shilingi bilioni 3 kila moja, salio lako litabaki bilioni 103.

TENGA FEDHA YA MATUMIZI

Kutokana na kiasi kilichobaki jiwekee matumizi ya shilingi milioni moja kila siku kwa miaka 80 ijayo utakuwa umetumia kiasi kisichozidi bilioni 30 na hivyo kulifanya fungu lako kusalia na bilioni 73.

Hata kama ukiamua kuwanunulia bia na nyama choma washikaji zako kila siku za shilingi laki 3 kwa miaka 80 ijayo huwezi kumaliza shilingi bilioni 10 na hivyo kubaki na kiasi cha bilioni 63 ambazo unaweza kuamua kufanya kufuru yoyote ya matumizi mtaani na watu wakashangaa.

TUTAFAKARI PAMOJA

Kama ikithibitika kuwa ‘dogo’ atakuwa amejipatia kiasi hicho cha fedha inatosha kuamini hilo bila kujiuliza amezifanyia nini hapa mjini? Kwa kuwa mambo haya yako mbele ya mahakama si vyema kuyajadili sana badala yake tusubiri haki itendeke ndipo tutakapokuwa na uwanja mpana wa kutafakari upotevu huu mkubwa wa fedha ambao serikali inadai kuibiwa.

TUHUMA ZA KAMBANGWA

Mfanyabiashara Kambangwa, Ijumaa iliyopita alifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, akikabiliwa na mashtaka manne likiwemo la kukwepa kodi na kujipatia Sh.bilioni 188.9 kupitia mashine ya kieletroniki (EFD).

Mwendesha mashtaka wa serikali Mwandamizi, Christopher Msigwa, akimsomea mashtaka mbele ya Hakimu Mkazi Janeth Mtenga, amedai kuwa katika siku tofauti kati ya Juni Mosi, 2016 na Novemba 2, 2018 Kambangwa alijifanya mtu aliyesajiliwa kuwa wakala wa kodi ya ongezeko la thamani (VAT) na kukusanya kodi ya VAT Sh.188,928,752,166 akidaiwa kufanya hivyo kwa niaba ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Katika shtaka la pili, mtuhumiwa amedaiwa kati ya Juni Mosi, 2016 na Novemba 2, mwaka huu, kwa udanganyifu alitumia mashine ya kieletroniki (EFD) yenye namba 03TZ842011315 iliyosajiliwa kwa jina la Kampuni ya Abraham’s Group LTD kukwepa kodi ya VAT yenye thamani ya kiasi hicho cha fedha.

Aidha mshtakiwa amedaiwa kuwa katika tarehe na kipindi hicho alijipatia au kujimilikisha fedha hizo alizozipata kutokana na makato ya kodi ya VAT ambazo zilipaswa kutolewa kwa kamishna wa TRA, ikadaiwa mshitakiwa alitenda kosa hilo huku akijua kuwa fedha hizo ni zao la kosa tangulizi la ukwepaji kodi.

Aidha imedaiwa kuwa mshtakiwa kwa vitendo vya makusudi vya kukwepa kodi alitumia mashine ya EFD na huku akijua kwamba hajasajiliwa kama mlipa kodi ya VAT na aliisababishia hasara Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ya Sh. 188,928,752,166.

Hata hivyo, mshtakiwa hakuruhusiwa kujibu chochote mahakamani hapo kwa kuwa mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu haina mamlaka ya kusikiliza kesi za uhujumu uchumi isipokuwa kwa kibali kutoka kwa DPP. Wakili wa Utetezi, Shamo Shadrack, aliiomba mahakama kupanga tarehe ya karibu ili kupinga mashtaka hayo dhidi ya mshtakiwa na kesi hiyo imeahirishwa hadi Desemba 17, mwaka huu kwa kuwa upelelezi wake haujakamilika.


Loading...

Toa comment