The House of Favourite Newspapers

KUHARIBIKA KWA CHUJIO ZA FIGO (GLOMERULONEPHRITIS)

KUHARIBIKA kwa chujio kitaalam glomerulonephritis ni aina ya ugonjwa wa figo unaoathiri sehemu maalum ya figo (chujio) inayohusika na uchujaji wa maji na uchafu kutoka katika damu. Sehemu hii huitwa glomelurus au chujio kama tutakavyokuwa tukitumia katika mada hii.

VISABABISHI

Mara nyingi chanzo halisi cha kuharibika kwa chujio za figo (glomerulonephritis) huwa hakijulikani. Hata hivyo, wakati mwingine uharibifu huu unaweza kusababishwa na kushambuliwa na mfumo wa kinga ya mwili. Uharibifu katika chujio husababisha damu na protini kuingia kwenye mkojo.

Tatizo hili hukua kwa haraka na figo inaweza kupoteza uwezo wake wa kuchuja maji na uchafu kwa kasi ndani ya muda mfupi wa kati ya wiki chache mpaka miezi kadhaa. Aina hii ya kuharibika kwa chujio za figo kwa haraka hujulikana kitalaam kama rapidly progressive glomerulonephritis.

UKUBWA WA TATIZO NA VIHATARISHI VYAKE

Takriban robo ya watu wanaopatwa na tatizo sugu la glomerulonephritis huwa hawana historia ya kuwa na ugonjwa wowote wa figo hapo kabla.

Kuna mambo kadhaa yanayoweza kumfanya mtu awe katika hatari ya kupata glomerulonephritis. Mambo hayo ni pamoja na matatizo katika mfumo wake wa damu au lymph, kuwahi kutumia vimiminika vilivyotengenezwa kwa kemikali za hydrocarbon, wenye historia ya saratani na maambukizi ya bakteria aina ya streptococcus, virusi, majipu au maambukizi katika moyo.

Mambo mengine yanayoweza kuongeza hatari ya kupatwa na glomerulonephritis ni pamoja na magonjwa ya mishipa ya damu kama vile vasculitis au polyarteritis, matumizi yaliyopitiliza ya dawa za kutuliza maumivu za jamii ya non-steroidal anti-inflammatory drugs kama vile aspirin na magonjwa ya mfumo wa kinga ya mwili kama vile anti-glomerular basement membrane antibody disease na iga nephropathy.

Mambo mengine ni makovu katika chujio (focal segmental glomerulosclerosis) au hali ya chujio kuwa na kuta nene kuliko kawaida (membranoproliferative GN), magonjwa yanayoathiri viungo mbalimbali vya mwili kama vile Henoch-Schonlein purpura, Goodpasture’s syndrome au Lupus nephritis na ugonjwa wa kimetaboliki wa amyloidosis.

DALILI

Dalili kuu za kuharibika kwa chujio au glomerulonephritis ni kuwa na damu katika mkojo (hali inayoufanya mkojo kuwa na rangi kama nyeusi, kutu au samawati; mkojo kuwa kama wenye povu jingi (kwa sababu ya kuwa na protini nyingi kuliko kawaida) na kuvimba uso, macho, miguu au tumbo (hali inayojulikana kama edema). Ukiona dalili hizo nenda kaonane na daktari wako akupime na kukupa dawa sahihi na utapona

Comments are closed.