The House of Favourite Newspapers

KUJIVUA NGUO KWA LUGOLA, KUCHEPUKA KWA RC GUMZO!

KAULI mbili za viongozi wa Serikali, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Albert Chalamila na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola zimeibua gumzo la aina yake. 

 

Mkuu huyo wa mkoa alimwambia Rais Dk John Pombe Magufuli kuwa anampa mshahara unaomtosha hata kuwa na mchepuko kidogo. Kwa upande wake Waziri Lugola aliliambia Bunge wiki iliyopita kuwa endapo ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad itakuwa ni kweli, yupo tayari kuvua nguo ikibainika kuwa taarifa zake za ukaguzi kuhusu sare hewa za Jeshi la Polisi zilizogharimu shilingi bilioni 16 ni za kweli.

 

RC CHALAMILA

RC Chalamila yeye alimwambia Rais Magufuli kuwa ataendelea na msimamo wake katika kuhakikisha anasimamia sheria ili shughuli za maendeleo ziweze kufanyika katika Jiji la Mbeya. Alisema amekuwa akiingia majaribuni mara kwa mara hususan kupitia watu wenye vipato vikubwa kwa nia ya kumuhonga, lakini amekuwa akiwaagiza wapeleke fedha hizo kwenye miradi ya maendeleo hasa mashuleni.

“Tukisimamia sheria tutalifikisha taifa hili mbele, inasikitisha kuona baadhi ya viongozi wanaleta unafiki katika kusimamia sheria, hii siyo nzuri hata kidogo,” alisema Chalamila na kuongeza: “Tangu Rais Magufuli aliponiteua sijawahi kukaribisha kiumbe chochote kije kinipe utajiri mfukoni mwangu, watu walionesha nia, nikawaambia wapeleke kwenye mashule, lakini mshahara ninaopata unatosha kukaa hata na mchepuko kidogo.”

 

Kwenye mitandao ya kijamii, ishu hiyo iliibua mjadala mzito kwani wakati anazungumza maneno hayo kulikuwa na watoto na viongozi wa dini kama kwamba ni jambo zuri kwenye jamii. “Kumbe ndivyo wanavyotumia fedha za walalahoi wanaolipa kodi? “Maskini walimu wanateseka wakati yeye analipwa hadi anapata za za ziada za kuweza kumpa mchepuko.

 

“Ukiwa kiongozi unapaswa kuwa na busara ya kujua useme nini na wakati gani mbele ya hadhara, sasa kauli yake inafundisha nini kwa jamii? “Yaani mkuu wa mkoa kabisa anatangaza kuweza kuwa na mchepuko, hii ni aibu,” zilisomeka baadhi ya ‘komenti’ nyingi kuhusiana na kauli hiyo ya RC Chalamila. Hata hivyo, mwenyewe alisema alitoa kauli hiyo katika hali ya utani.

 

WAZIRI LUGOLA

Kwa upande wake, Waziri Lugola yeye alisema hajawahi kumuona mtu muongo katika nchi hii kama CAG. Alisema anauweka rehani uwaziri wake ikiwa itathibitika kuwa taarifa za ukaguzi wa CAG kuhusu sare hewa za Jeshi la Polisi zinazofikia shilingi bilioni 16 ni za kweli.

 

“Sijawahi kuona mtu muongo kama CAG, Jeshi la Polisi hakuna sare hewa. Ninaomba Maafisa wa Ofisi ya CAG twende nao stoo wakaone sare mpya za Jeshi la Polisi. Kama nasema uongo, nitavua nguo na ninaweka uwaziri wangu rehani.”

 

Kauli hiyo nayo iliibua gumzo kubwa huku baadhi wakidai wanatamani kumuona akivua nguo kutokana na lile umbo lake la miraba minne. “Alichokisema CAG ni kwamba kukosekana kwa nyaraka za kuthibitisha uletaji wa mzigo ndipo penye tatizo.

“CAG alisema aliomba hati ya kupokelea shehena ya mzigo bandarini (bill of lading), hati ya madai kutoka kwa mtengenezaji (commercial invoice), hati ya mzigo ulipotoka (certificate of origin), orodha za mali zilizopo kwenye meli (packing list) na cheti cha ukaguzi wa bidhaa (inspection certificate), kutoka kwa Mzabuni Daissy General Traders kwa ajili ya kujiridhisha kama bidhaa husika zililetwa nchini, lakini vyote hivyo havikuwepo.

 

“CAG alisema alipitia Mfumo wa Forodha (TANCIS) wa Mamlaka ya Mapato (TRA) na kubaini kuwa hapakuwa na shehena yoyote kutoka kwa Mzabuni Daissy General Traders.

 

“Sasa Waziri Lugola hakutakiwa kusema atavua nguo bali ni kutoa tu documents (nyaraka) ili kumaliza utata…” ilisomeka sehemu ya maoni mengi kwenye ukurasa wa Global Publishers kwenye Mtandao wa Instagram.

 

Hata hivyo, baadhi ya wachangiaji juu ya maadili ya viongozi wa Serikali walimtaka Waziri wa Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Mkuchika kufanya kazi kubwa ya kusimamia maadili ya viongozi wa umma.

Comments are closed.