The House of Favourite Newspapers

KUKU WA KIENYEJI YAKE PUMBA

KAMA nakuona unavyotikisa kichwa na kujiuliza leo Anti ameleta kuku na pumba tena? Na utatikisa kichwa na mijicho kuitoa sana mwaka huu! Jitu zima hoooovyoooo kutwa kumkosesha amani mkeo! Shuutuuuuu!

Shoga leo nina hasira, limenifika hapa, mpaka nimebanwa na kwikwi! Ujue kwa nini? Kuna wababa watu wazima na midevu yao lakini ukiwaona tabia zao kama vile watoto wadogo! Mbaya zaidi wababa hao wanakutana na wanawake wenye kujiheshimu, wenye kukaa kimya hata wakitendwa! Jamaaaniiii! Yaani mpaka nahisi moyo wangu unashindwa kudunda kwa presha niliokuwa nayo!

Juzi nimepata ujumbe kutoka kwa msomaji mmoja wa kona yetu hii kuwa amezidiwa matatizo hadi inafikia kipindi anatamani tu apotee duniani! Nimejitahidi sana kumue-lewesha na kumpa elimu akanielewa. Aliniambia kuwa mume wake alikutana naye kwa mara ya kwanza kwenye harusi ya shoga yake, kuanzia hapo wakawa marafiki na haikuchukua mwaka akaolewa.

Baada ya kuolewa alibahatika kupata mtoto mmoja ikabidi atafute dada wa kazi vijana wa leo wanawaita kuku wa kienyeji sijui! Basi shoga, ndani ya mwezi tu huyo dada wa kazi akaanza kubadilika taratibu mara mwili, sura, matendo, tabia, mikogo loooo! Hadi kwa mumewe akambadilikia akaanza kutembea naye!

Bora basi angetembea naye kimyakimya, si akaanza kujianika na kumuoneshea dharau, mara akiambiwa kufua anasusa, kupika ndo kwanza domo analirefusha kama fundi bomba aliyeshindwa kurudishia bomba linalomwaga mwaji kwa presha ya juu!

Wakati mwingine nikisema sisi wanawake sijui akili zetu huwa anatushikia nani huwa namaanisha ati! Ona tunavyodharaulika kwa vitu kama hivi, hujui watu walipotokea, mwenzako amefunga ndoa ya kidini tena iliyofuata misingi yote wewe kirahisi unakuja kubomoa, unajua alilipiwa mahari kiasi gani? Unajua aliambiwa nini kwenye kicheni pati?Picha inayohusiana

Nikugeukie na wewe mwanaume! Jitu zima umekazania kuku wa kienyeji aliyezoea pumba! Jamani hawa wadada wa kazi kazi yao siyo kuishi na mume wa mtu, sawa unaweza kumgeuza kuwa sehemu ya ndugu lakini muwe mnaangalia na mipaka ati, uongo?

Kwanza kutembea na wanawake wa aina hii ni kumdharau mkeo, wewe mwenyewe pia mpuuzi, heshima ya nyumba siyo kutembea na dada wa kazi! Kuna msemo unaosema mwanamke mpumbavu hubomoa nyumba yake kwa mikono yake mwenyewe! Binafsi napingana nalo, kuna wanaume wapumbavu ambao nao hubomoa nyumba zao tena kwa mikono hiyo miwili na akili juu, upo?Shoga nikiongea sana naona kama nitachafua hali ya hewa tu hapa! Tukutane tena wiki ijayo kwa mada nyingine nzuri.

Ni mimi Anti Naa Shangingi Mstaafu.

 

 

Comments are closed.