The House of Favourite Newspapers

 KUKUAMBIA ANAKUPENDA PEKEE HAITOSHI IKIWA…

MPENZI wako anapokuambia anakupenda, inatosha kweli kukudhibitishia kuwa anakupenda kwa dhati na uendelee kumwamini? Hapa kila mmoja anaweza kuwa na jibu lake, lakini kwa wataalamu wa uhusiano hawakubaliani na hoja hii.  Kwanini? Kwa sababu neno ‘nakupenda’ ni jepesi sana katika hali ya kawaida kutamkika, lakini lina maana kubwa sana linapokuja katika ulimwengu wa mapenzi ya dhati. Naam! Ulimwengu wa mapenzi ya dhati kwa sababu kuna wengine wanakuwa hawana mapenzi ya kweli wanapotamka neno hili. Wanasaikolojia ya mapenzi wanaeleza kwamba neno hilo linaweza kuwa na maana ikiwa litalandana na matendo.

Wengi wamekuwa wakiteseka kwa muda mrefu katika uhusiano. Wapenzi wao wamekuwa hawaeleweki kama wana mapenzi ya kweli au lah, kutokana na mambo wanayowafanyia lakini kwa wakati huo huo neno ‘nakupenda’ limekuwa halikauki midomoni mwao.

Ni haki yao kuchanganyikiwa, lakini kuchanganyikiwa huko kutokana na kutokujua mambo ya uhusiano vyema. Inawezekana wewe ukawa mmoja wa watu hao, hii ni nafasi yako mahususi kwa ajili ya kumfahamu mpenzi wako vyema. Je, anakupenda? Fuatilia vipengele vifuatavyo ili uweze kupata ufahamu.

ANAKUPUUZA

Hili ni tatizo kubwa katika uhusiano na hasa wanaonyanyaswa na hili ni wasichana. Wanaume wengi wa siku hizi ambao wana mapenzi ya ubabaishaji huwapuuza wenzi wao. Hivi utawezaje kukubali kuendelea kuitwa mpenzi na kila wakati mtu huyo anakuambia anakupenda lakini anakupuuza? Bado utaendelea kumhesabia mtu huyo anakupenda? Kwa lipi hasa wakati hazingatii yale umuambiayo hata kama yana msingi kiasi gani katika maisha yenu yajayo?

Mpenzi mwenye mapenzi ya kweli kwanza huzingatia mawazo ya mpenzi wake, hupima kila aambiwalo na kulifanyia kazi. Huwezi kumpuuza mtu ambaye unampenda hata siku moja. Hiki ni kipimo cha kuzingatia wakati unatafuta mpenzi wa kweli. Hata kama anakuambia anakupenda mara ngapi kwa siku, lakini kama haonyeshi kuthamini umuambiayo, penzi la mtu wa aina hii lina mushkeli.

Anayekupenda huwa makini kukusikiliza kwa kila kitu. Mwingine anaweza akawa anamshauri vizuri sana juu ya maisha lakini mwanaume huyo akawa hana time kabisa naye, usingoje kujidhalilisha zaidi ya hapo, huyu atakuwa hakupendi ila ana vitu anavyovipata kwako ndiyo maana anajilazimisha kukuambia ‘nakupenda’ ya kinafiki ili aendelee kupata anachokipata kutoka kwako. Upo hapo?

ANAHOFIA SIMU YAKE

Hapa kuna utata mkubwa! Wengi hujitetea kuwa simu ya mkononi ni kwa ajili ya mhusika na sio vinginevyo, hapa kuna ukweli fulani lakini wengi walio katika uhusiano hutumia kijisababu hiki kama nguzo ya kuendelea kufanya mambo yao yasiyofaa kwa kutumia simu zao.

Hata hivyo wanasaikolojia ya mapenzi wanaunga mkono hoja hiyo, maana wakati mwingine unaweza ukachukua simu ya mpenzi wako na ikasababisha mgogoro mkubwa. Pamoja na hilo, kumgundua mwizi ni rahisi sana, ukikutana naye hata kama humfahamu unaweza ukajikuta unamhisi, ndivyo ilivyo katika uaminifu wa simu za mikononi. Ukiona umeshika tu simu yake anakuwa mkali, jua kuna kuna kitu kinaendelea.

Simu inapigwa halafu ghafla anatoka kwenda kupokelea nje, jiulize mara mbili. Lakini wakati mwingine ukiona simu yake inaita halafu jina linalotokeza kwenye simu yake lina utata, anza kufikiria mara mbili. Kwa mfano ukiona jina limeandikwa kwa vifupisho au majina yasiyoeleweka, jua kuna mambo yanaendelea chini ya kapeti.

Ukianza kuhisi tofauti kidogo juu ya simu yake, anza kumchunguza na mara nyingi akigundua unamchunguza kuliko umharibie mambo yake atakuwa tayari kuachana na wewe. Kukuambia anakupenda pekee hakutakuwa na maana kukiwa na kasoro hii. Alhamisi ijayo tutaendelea na mada hii, USIKOSE!

Joseph Shaluwa ni Mshauri wa Uhusiano anayeandikia Magazeti ya Global Publishers. Ameandika vitabu vingi, vikiwemo True Love, Let’s Talk About Love na Maisha ya Ndoa vinavyopatikana kwa oda. Kwa sasa anaandaa kitabu chake kipya cha SIRI ZA NDOA YENYE FURAHA kitakachotoka hivi karibuni

 

Comments are closed.