KUKUAMBIA ANAKUPENDA TU HAITOSHI IKIWA… – 2

TUNAMALIZIA mada yetu iliyoanza wiki iliyopita. Muhimu tunaangalia kasoro unazotakiwa kuziangalia kwa mpenzi uliyenaye. Je, upo kwenye uhusiano na mpenzi wa aina gani?  Anaweza kuwa anakuambia mara nyingi ‘anakupenda sana’, lakini je, inaweza kuwa kipimo cha penzi la dhati kwako? Tuendelee na vipengele vilivyosalia.

 

HATAKI KUKUTAMBULISHA

Kukupenda kwake hakuwezi kukamilika ikiwa hataki kukutambulisha. Ni kweli kwamba jambo hili siyo la haraka, lakini unaweza kukuta wapenzi wapo katika uhusiano kwa mwaka mzima au zaidi lakini hakuna ndugu yeyote wa upande wa mwanaume anayemfahamu!

 

Ukiachilia mbali ndugu zake lakini hata marafiki zake wa karibu hawamfahamu, hilo ni tatizo. Kwa hali kama hiyo hata kama jamaa atakuwa akirudia kusema anakupenda mara ngapi, haina maana. Fanya maamuzi tusiyape nafasi mapenzi yatuumize mioyo yetu. Pindi unapoona mpenzi wako haeleweki, anza kumchunguza mara moja; mwekee mitego, muulize maswali mengi yanayokutatiza, hapo utaujua ukweli na utaamua kunyoa au kusuka!

HAYUPO HURU KWAKO

Mpenzi wa aina hii atakuwa na ‘nakupenda’ nyingi sana mdomoni mwake, lakini hayupo huru kabisa kwako! Siku zote huwa mnakutana chumbani tu na hata kama siyo chumbani labda mmepanga kutoka basi mtakutana huko huko. Hapendi kuongozana na wewe na huwa na visingizio kibao. Anaweza kukuambia mkutane mahali fulani na kama ukipendekeza muongozane atakataa na kukupa visingizio visivyo na msingi.

 

Mbaya zaidi mnaweza kuwa pamoja na mkaamua kwenda mahali fulani, bado atang’ang’ania utangulie hatua kadhaa au yeye atangulie halafu wewe ufuate nyuma! Kwa nini? Kuna tatizo, anaona hana hadhi ya kuwa na wewe, anakudharau lakini anashindwa kuachana na wewe kwa sababu ana mambo yake anayoyapata kutoka kwako.

 

Hapo unapaswa kuzinduka, kuchekecha ubongo wako na kuchukua hatua. Kama anakupenda kwa nini anashindwa kuongozana na wewe, kwa nini anakataa msiwe pamoja kwenye hadhara, anamwogopa nani kama siyo hakupendi? Fikiria zaidi!

 

HAKUSHIRIKISHI

Mpenzi wa aina hii, hashindwi kukuambia anakupenda wakati mwingine hata mara tatu au zaidi kwa siku lakini kamwe hakushirikishi katika mambo yake.

 

Hataki kukuambia na anaonyesha wazi wazi kuwa hapendi kukushirikisha. Hata kama utaonyesha dalili za kutaka kujua mambo yake na kumsaidia hata mawazo, hataonyesha kufurahia jambo hilo, mara nyingi anataka kufanya mambo yake kwa kificho bila kuingiliwa maamuzi yake.

 

Utakapohitaji kumsaidia atakuambia mambo yanayomhusu yeye umuachie mwenyewe. Hili ni tatizo tunapozunguzia mapenzi ya dhati. Wapenzi siku zote hushirikiana. Kama hataki kukushirikisha, kuna maana gani yeye kuendelea kukuimbia wimbo wa ‘nakupenda’ kila wakati?

USIUTESE MOYO WAKO

Kukuambia anakupenda kila wakati hakuwezi kukuthibitishia kuwa ana mapenzi ya kweli ikiwa kuna kasoro nilizoanisha hapo juu. Ikiwa kasoro zote zipo na ukafanya uchunguzi na kugundua kuwa jamaa hakupendi, usiteseke zaidi! Chukua hatua, epusha matatizo katika moyo wako, upe haki ya kuwa furaha, unapaswa kufurahia mapenzi na siyo kutesekea mapenzi!

 

Katika hali kama hii ni sahihi kuchukua hatua ya kuokoa mateso moyoni mwako. Hadi wiki ijayo kwa mada nyingine kali, USIKOSE!

Joseph Shaluwa ni Mshauri wa Uhusiano anayeandikia Magazeti ya Global Publishers. Ameandika vitabu vingi, vikiwemo True Love, Let’s Talk About Love na Maisha ya Ndoa vinavyopatikana kwa oda. Kwa sasa anaandaa kitabu chake kipya cha SIRI ZA NDOA YENYE FURAHA kitakachotoka hivi karibuni.

Toa comment