The House of Favourite Newspapers

Kulia kwa Ajili ya Mapenzi si Kutatua Tatizo

Mwanamke akili chumbani.

KARIBU mpenzi msomaji wa Sindano za Mastaa, wiki iliyopita ulikuwa na staa wa Bongo Fleva, Dayna Nyange lakini wiki hii upo na staa wa sinema za Kibongo, Jacqueline Wolper ambaye anakupa tumaini jipya wewe ambaye umeumizwa na umelizwa kwa sababu ya mapenzi.

Jambo muhimu la kujifunza kutoka kwa Wolper ni wewe kufuta machozi ya mapenzi na kusimama imara kwa ajili ya maisha mengine.

Mapenzi yanatesa, yanaliza na yanakwaza zaidi ya kitu chochote katika dunia hii. Kama mwanadamu, kama mwanamke, nilishaumizwa, nimeshatendwa na mtu ambaye nilimpenda. Niliumizwa lakini mwisho wa siku niligundua kuwa kuna maisha nje ya machozi ya mapenzi, nikaamua kuamka kiakili na kuanza kusonga mbele na hadi leo mimi ni miongoni mwa mastaa ambao ni nembo ya Tanzania katika sinema za Kibongo.

Kwa nini wewe uendelee kulia na kung’ang’ania kuwa huwezi kuishi bila huyo aliyekuumiza? Mtu amekuumiza lakini bado unahangaika naye wa nini? Huyo hakufai katika maisha yako, huyo ni adui wa maisha na maendeleo yako, futa machoni na uukubali ukweli kama mapenzi yenu yameisha.

Kwani huwezi kufanikiwa au kufikia jambo fulani kama una maumivu ya mapenzi moyoni mwako au una kovu la kidonda cha mapenzi. Mafanikio yanahitaji amani ya moyo.

Ulipoteza matumaini ya kupenda au kupendwa kwa sababu ya mtu mmoja ambaye ulimpenda lakini yeye hakukupenda, akaja kukuumiza, kukuliza na hata kukuacha, lakini leo nakuambia simama na uendelee na safari yako.

Katika safari ambayo unaianzisha unaweza kufika unapotaka bila mtu mwingine lakini ninachoamini kabla hujafika au kumaliza safari yako kuna msaidizia mwema na mwenye upendo wa dhati utampata na kukusaidia au kukufikisha mwisho wa safari yako.

Kama mwanamke nimepitia mambo mengi sana kwenye mapenzi, wapo walionilaghai kwa sababu ya uzuri wangu, wapo walionitamani na kuniacha solemba. Nimelia, nimeumizwa ila mwisho wa siku nilijitambua kuwa mimi ni nani na ndiyo maana leo hii niko hapa nilipo.

Hamu yangu ni kukuona na wewe ukifuta machozi na kupigania ndoto zako. Makala haya nimeyaandika maalumu kwako wewe ambaye umewahi kuumizwa, kulizwa, kuteswa, kusimangwa, kudhalilishwa, kufedheheshwa kwa sababu ya mapenzi.

Achana na mambo ya kale, futa machozi, anza safari nyingine ya mafanikio katika maisha yako, aliyekuumiza si baba wala mama yako, yeye siyo pumzi au uhai wa maisha yako kusema kwamba bila yeye huwezi kuishi.

Amini aliyekuacha yeye si maji ya kunywa kusema kwamba atakata kiu yako, si chakula kusema atashibisha tumbo lako na wala si tabibu kusema atarudisha upya afya yako kwa mateso aliyokusababishia.

Simama imara,  nyanyuka mwanamke mwenzangu, songa mbele, hakikisha unatimiza ndoto zako. Usinione mimi nimefika hapa, nimepitia vishawishi na vizingiti  vya kila aina, kuna wakati changamoto zina kuzidi na kuamua kujifungia ndani pekee yako na kuanza kulia lakini haisaidii kitu. Bali kufuta machozi na kujipanga upya ndiyo njia sahihi ya kukabiliana na tatizo.

Leo nitaishia hapa mpenzi msomaji, ila nakaribisha ushauri na maoni yako.

Comments are closed.