The House of Favourite Newspapers

Kumbe Aliens wamekuwepo enzi na enzi!

0

AliensILIPOISHIA WIKI ILIYOPITA:
Mpenzi msomaji wangu wiki iliyopita tuliona ni kwa jinsi gani hawa viumbe wa ajabu waishio angani wa Aliens walivyo na tabia zinazoaminika ni za majini japokuwa wana utofauti kidogo. Tuliona kuwa tofauti kubwa iliyopo kati ya Aliens na majini ni kwamba majini wana maumbile maalum na uwezo wa kujibadilisha japo wote wana uwezo wa kusafiri kwa kasi ya upepo. SASA ENDELEA…

Kama nilivyoeleza awali katika matoleo ya simulizi hii huko nyuma, kuna filamu na tamthiliya mamilioni duniani zinazozungumzia viumbe hawa wa Aliens na madhara yake ambayo hata hivyo, hayaelezwi yatamsababishia nini mwanadamu.

Baadhi ya filamu na tamthiliya hizo ni pamoja na Star Wars, Star Trek, Men In Black II, From the Earth to the Moon, Apollo 13, War of the Worlds na X-Files. Cha ajabu mara nyingi kiongozi au mhusika mkuu wa kwenye sinema hizo husemekana ni mtu wa jamii ya siri ya Freemasonry.

Inadaiwa kuwa ndiyo maana kwenye sinema hizo huwa na alama nyingi za Freemasons. Wapo wanaoamini watengenezaji hufanya hivyo kulenga biashara.Wengine huamini kuwa sinema hizo huwafanya wanadamu wawaze kama wanavyotaka maadui zao wanaaminika ni hao Aliens.

Kwa mfano; kwa wale waliobahatika kufuatilia au kutazama Sinema ya Men in Black II watakubaliana na mimi kuwa inazungumzia serikali ya siri ambayo kazi yake kubwa ni kuwalinda wanadamu kutokana na tishio la viumbe hao kutoka nje ya sayari hii ya dunia.

Pia ipo Filamu ya Deep Impact inayozungumzia vimondo vinavyoanguka kwenye uso wa dunia yetu vikiwa ni sehemu ya vitisho vya wanadamu kutoka sayari nyingine.

Kuna wanaoamini suala la viumbe hawa ni ndoto za wasiomwamini Mungu na kuna wenye shauku ya kutaka kupata elimu zaidi. Pia wapo wanaoamini kwamba kama kitu hakijaandikwa kwenye vitabu vitakatifu ni uongo uliokithiri kwa sababu viumbe wote wameumbwa na Mungu. Wanaamini kuwa hakuna viumbe wengine zaidi ya binadamu, malaika, wanyama, ndege, wadudu na majini.

Kuhusu uwepo wa Aliens, kama nilivyoeleza wakati naanza simulizi hii, mimi sina ushahidi wa kutosha wa kuhitimisha kuwa viumbe hao wapo hivyo kwa wale ambao mmekuwa mkiniuliza juu ya msimamo wangu ndiyo huo.

Tunapojikita katika simulizi za ziara za viumbe hawa kuja duniani, nami naamini inawezekana hazina ukweli wowote bali ni upotoshaji na hila tu za binadamu wanaotaka kuteka dunia kifikira.

Kuonekana kwa Aliens na vyombo visivyotambulika vipaavyo angani (UFO), si jambo la ajabu kwani ni kweli vimeendelea kuonekana duniani tangu enzi na enzi lakini hakuna ushahidi wa moja kwa moja wa kusema kwamba ni viumbe hawa wa Aliens kwani ikiwa hujatambua ulichokiona basi hufahamu ulichokiona. Kama hujui unachokiona huwezi kujua ulichokiona.

Katika mazingira kama hayo, watu wamekuwa wakitengeneza simulizi nyingi zilizojaa uongo wenye lengo la kuchochea au kuhalalisha mambo wasiyojua.

Ukweli ni kwamba UFO nyingi huwa ni vifaa vya kiusalama vya majeshi ya nchi mbalimbali zilizoendelea duniani ambavyo watu huhusisha na viumbe kutoka sayari nyingine.

Hata hivyo, mbali na Aliens lakini viumbe wasioonekana wapo wengi mno na bado kuna jamii kubwa sana ya bakteria na virusi ambavyo bado havijagundulika, labda kutokana na uchanga wa utafiti wa kibinadamu.

Hata kwenye hewa hii tunayoivuta tunaambiwa kuna idadi kubwa ya viumbe vidogo mno ambavyo si rahisi kuviona kwa macho.

Itaendelea wiki ijayo.

Leave A Reply