Kumbe rais mtarajiwa ndugu yangu kabisa

Yaani mimi mwenyewe bado sijaamini. Babu yangu ndiyo kaniita jana akaniambia hii siri kubwa ya kifamilia ambayo sasa ningependa kuwahusisha. Mara alipotangazwa mshindi wa mbio za urais babu yangu akaniita chumbani kwake, akaniambia, ‘Mjukuu wangu kuna siri nataka kukwambia. Sijui unajua kuwa baba yangu aliwahi kuishi Chato?’

Nikamjibu babu kuwa sikujua hilo. Basi babu ndiyo akaanza kunihadithia siri kubwa sana. Kumbe baba yake babu alikuwa anaishi Chato, jirani kabisa na baba yake wa babu wa prezda mteule, umenipata? Walikuwa wana kunywa pamoja, yaani walikuwa kloz sana. Mmoja akitaka kuchil lazima amtafute mwenzie.

Sasa binamu yake babake babu wa prezda, alikuwa kaoa kijiji cha jirani na pale Chato, sasa kutoka ukoo ule aliooa ndiyo babake baba si akazaa na binti mmoja, ilikuwa kesi kubwa na babake babu akatozwa faini ambayo kaka yake wa binamu yake wa babu yake wa prezda ndiye aliyekuwa mtetezi mkubwa wa baba yake babu yangu, hata ile faini alilipa yeye. Sijui umenipata mpaka hapo?

Huyu mtoto aliyezaliwa ambaye kimsingi ni babu yangu alipokuwa mtu mzima akamuoa mtoto wa kaka yake wa binamu yake babu wa prezda, sasa ukiangalia hapo utakuta kiukweli kabisa mi ni ndugu yake wa damu wa rais mtarajiwa.
Babu hakuishia hapo, aliniambia kuhusu kesi nyingine iliyohusiana na mgogoro wa kugombea shamba ambayo kaka yake wa binamu wa prezda aliingilia kati na kuimaliza haraka iwezekanavyo.

Babu aliniambia kwamba kule Chato kuna mzee mmoja alikuwa na shamba lililopakana na la babu ambaye shangazi yake aliolewa na bwana ambaye alikuwa na undugu na familia ya prezda mteule.

Aliongeza kuwa jamaa huyo kwa makusudi kwa vile mashamba hayo hayakuwa na mipaka, alikata kipande kikubwa cha ardhi na kudai kilikuwa eneo lake ndipo mgogoro ulipoibuka na kusababisha ndugu zake na wale wenye ukoo na prezda kununiana na kutoleana vitisho lakini kaka yake wa binamu yake babu wa prezda alimaliza mgogoro huo kwa amani.

Mara baada ya kuapishwa babu amesema atanipeleka ikulu kunitambulisha, kikubwa ni kutoa shukrani kwa ile faini iliyolipwa enzi zileee, unajua ndugu ni muhimu wafahamiane, inawezekana prezda akawa ana shida fulani basi anajua kuwa ndugu yake wa damu nipo, wala si kwa sababu nyingine yoyote. Siyo jambo zuri jamani?


Loading...

Toa comment